Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mpango wa jiolojia PanAfGeo unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, unatarajiwa kuzinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam, Tanzania Juni 24 mwaka huu 2025. Tukio hili muhimu linafuatia miaka minane ya utekelezaji na awamu mbili zilizopita za PanAfGeo, likionesha dhamira mpya ya kimkakati ya kuimarisha uwezo wa Afrika katika masuala ya jiolojia na kuendeleza ushirikiano kati ya mabara katika usimamizi endelevu wa rasilimali za madini na jiolojia.
PanAfGeo ni kifupi cha (Pan-African Support to Geological Sciences and Technology) mradi wa kipekee wa bara la Afrika unaolenga kuimarisha ujuzi na uwezo wa wataalamu wa jiolojia barani Afrika. Ulianzishwa mwaka 2016 kwa ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, na umefadhiliwa kwa sehemu na Tume ya Ulaya.
Kupitia PanAfGeo, zaidi ya wataalamu 1,700 wa jiolojia kutoka nchi 54 za Afrika wamepata mafunzo ya vitendo katika nyanja mbalimbali kama vile:
Mafunzo haya yamekuwa yakitolewa moja kwa moja barani Afrika, yakihusisha nchi 22 kama wenyeji wa warsha 72 tofauti. Awamu ya pili ya mradi huu (PanAfGeo-2) ilikamilika mwaka 2024, na sasa imeanzishwa awamu mpya iitwayo PanAfGeo+, inayotarajiwa kuendelea hadi mwaka 2029.

Tukio hili limeandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Tafiti za Jiolojia za Afrika (OAGS), shirika la taasisi za kijiolojia la nchi za Ulaya ,EuroGeoSurveys (EGS), na kuratibiwa na Taasis ya Jiolojia ya Ufaransa (BRGM) ambapo linatarajia kuwakutanisha pamoja jumla washiriki 100 kutoka taasisi za jiolojia, serikali, mashirika ya kikanda na ya kimataifa wanatarajiwa kushiriki.
Katika awamu hii mpya inalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa kuongeza mafunzo na ushirikiano wa taasisi za kijiolojia kati ya Afrika na Ulaya.
Alipozungumza balozi wa umoja wa Ulaya nchini Tanzania Christine Grau amesema kuwa wanafuraha kubwa kuona tukio hilo linafanyika Tanzania kwa mwaka huu.
“PanAfGeo+ ni mfano wa mshikamano wa timu ya Ulaya tukisukuma mbele sayansi, maendeleo endelevu na ushirikiano wa kweli. Tunajivunia kuanza awamu hii mpya hapa Tanzania,”
“PanAfGeo+ si mpango wa kisayansi tu – ni chombo cha kuleta mabadiliko. Tunabadilisha maarifa kuwa maendeleo na ushirikiano kuwa mafanikio,” alisema Tirza van Daalen, Rais wa shirika la taasisi za jiolojia kutoka nchi za ulaya (EGS).
“Ushirikiano huu unaonyesha malengo yetu ya pamoja – kuiwezesha Afrika kuongoza kwa maarifa, uimara na uendelevu,” alisema Rokhaya Samba Diene, Rais wa shirika la tafiti za jiolojia za Afrika( OAGS).

Tukio hilo linatarajia kuhusisha majadiliano ya Kitaalamu huku mada zitahusu ushirikiano baina ya mabara, uboreshaji wa ujuzi, na nafasi ya kijiolojia katika maendeleo endelevu ya Afrika.
Aidha pia mkutano Mkuu na uwasilishaji wa miradi ya nchi ambapo nchi za Tanzania, Rwanda, Uganda na Zambia zitawasilisha miradi mipya ya ushirikiano wa kitaifa.
PanAfGeo+ inaendana na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 pamoja na Mkakati wa Umoja wa Ulaya wa Global Gateway. Hili ni tukio muhimu kwa diplomasia ya kisayansi, usimamizi wa rasilimali, na ajenda za mabadiliko ya kijani barani Afrika.
Mpango huu unatekelezwa chini ya mwamvuli wa timu ya Ulaya “Team Europe”, ukileta pamoja wataalamu wa jiolojia kutoka nchi 11 wanachama wa Umoja wa Ulaya kama Ufaransa, Uholanzi, Poland, Finland, Slovenia na wengine.
