Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa matakwa ya kikatiba ya usawa wa kijinsia yanatafsiriwa kwa vitendo katika nyanja zote za maisha, ikiwa ni pamoja na elimu, ajira, uongozi na mifumo ya sheria.
Haya yamebainishwa leo Mei 29,2025 Jijini hapa katika kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Usawa wa Kijinsia kilichofanyika jijini Dodoma, kikilenga kutathmini mafanikio, changamoto na mwelekeo wa utekelezaji wa Mpango wa Mageuzi ya Usawa wa Kijinsia (2021–2027).
Akizungumza kwenye kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bw. Amon Mpanju, amesema serikali inatengeneza mifumo rafiki kwa wote,unayowezesha wanawake na wanaume kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Amesema kutokana na juhudi zote hizo mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanaonekana kushuka kufuatia ongezeko la uelewa wa jamii na ushirikiano mpana kati yake na wadau wa maendeleo.
Naye Mtakwimu na Mratibu wa Programu ya Kuwezesha Wanawake Kushiriki Uongozi na Usawa wa Kijinsia kutoka Wizara hiyo Alex Shayo, amesema kuwa kiwango cha ukatili wa kijinsia kimeshuka kutoka asilimia 40 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 27 mwaka huu, kutokana na ongezeko la elimu kwa umma na mwitikio wa jamii.
Shayo ameeleza kuwa ongezeko la taarifa za ukatili kwa vyombo vya sheria ni ishara ya uelewa na ujasiri uliojengeka miongoni mwa wananchi, huku akisisitiza kuwa bado changamoto kama mila potofu na mifumo dume vinahitaji kushughulikiwa kwa kina.
Kwa upande mwingine amesema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma kwa waathirika wa ukatili, ikiwa ni pamoja na kuanzisha madawati ya kijinsia katika vituo vya polisi, nyumba salama kwa manusura, na madawati maalum katika shule za msingi.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Bi. Lucy Uisso, alisema mafanikio yanaonekana kupitia ongezeko la kesi za ukatili wa kijinsia zinazofikishwa mahakamani, ambapo idadi kubwa ya watuhumiwa wamekuwa wakitiwa hatiani, hali inayoonesha kuwa haki inatendeka kwa wahanga.
Kwa upande wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Abeida Abdallah, alibainisha kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN Women) na Umoja wa Ulaya imeendelea kutoa mafunzo kwa watendaji ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa manusura wa ukatili wa kijinsia.
Katika upande wa ushirikiano wa kimataifa, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Utawala Bora katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Karina Dzialowska, alieleza kuwa EU imetenga jumla ya Euro milioni 90 kwa utekelezaji wa Mpango wa Mageuzi ya Usawa wa Kijinsia, ambapo zaidi ya Euro milioni 28 zimeelekezwa moja kwa moja kwenye bajeti ya serikali ya Tanzania.
Amesema Mpango huo wa miaka saba unalenga maeneo muhimu kama vile Kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi,kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha na mikopo,kupambana na vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni,na kujenga uwezo wa wanawake kupitia TASAF na mashirika kama Pastoral Women’s Council (PWC) na Kanisa la Kilutheri Tanzania (ELCT).

Ameeleza kuwa mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/22–2025/26) pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, ambazo zote zimeweka usawa wa kijinsia kuwa miongoni mwa vipaumbele vya taifa.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimewakutanisha zaidi ya washiriki 65 kutoka serikalini, sekta binafsi, taasisi za kiraia, na wafadhili wa maendeleo, mjadala mkubwa ulijikita kwenye namna bora ya kuimarisha mifumo ya kisheria na kisera inayolenga kulinda haki za wanawake na watoto.
Aidha Serikali imesisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia si jukumu la serikali pekee bali ni la jamii nzima, na hivyo kuitaka kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kubadili mitazamo kandamizi, kuhimiza usawa na kujenga taifa lenye haki sawa kwa wote.