📌Kuhusisha Mifumo ya umeme jua 20,000 katika visiwa 120
📌Rais Samia awawekea wananchi ruzuku hadi ya asilimia 75 kuunganisha umeme
📌Mhe.Salome asema Serikali itafikisha umeme kwa wananchi bila kujali umbali na mtawanyiko wa makazi
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amezindua mradi wa kusambaza mifumo ya umeme jua visiwani unaolenga kuweka mifumo 20,000 ya umeme jua katika visiwa 120 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 8 ambapo Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka ruzuku hadi ya asilimia 75 katika gharama za uunganishaji umeme.
Mhe. Salome Makamba amezindua mradi huo katika kisiwa cha Bezi wilayani Ilemela mkoani Mwanza ambapo mradi huo unatekelezwa chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
“Maeneo ya visiwani na delta yana changamoto za kipekee, zikiwemo umbali kutoka Gridi ya Taifa, gharama kubwa za usafirishaji wa vifaa na mtawanyiko wa makazi unaoongeza gharama za usambazaji wa nishati ya umeme. Hata hivyo, changamoto hizi haziwanyimi wananchi haki ya kupata huduma ndio maana Serikali imekuja na mpango huu mahsusi wa matumizi ya mifumo ya umeme jua pamoja na gridi ndogo kama suluhisho la haraka la kuwafikia wananchi wa visiwa na maeneo ya pembezoni.” Amesema Mhe.Salome
Ameeleza kuwa hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa umeme katika maeneo kama hayo ya visiwa ni pamoja na kutoa ruzuku kwa mifumo ya umeme jua ili kuharakisha upatikanaji wa nishati safi, kupunguza utegemezi wa vyanzo visivyo endelevu kama dizeli, na kuhakikisha gharama za nishati zinakuwa nafuu.
Amesema mradi huo aliouzindua una mchango wa moja kwa moja katika kukuza Uchumi wa Buluu, ambao ni kipaumbele cha Taifa katika maeneo ya pwani na visiwa kwani mifumo ya umeme jua inayofungwa itawawezesha wavuvi kuongeza thamani ya samaki na dagaa kabla ya kupelekwa sokoni, jambo litakaloongeza mapato ya wananchi, Halmashauri pamoja na nchi, kuimarisha shughuli za ufugaji wa samaki (aquaculture), kilimo cha mwani, na huduma za utalii wa fukwe na visiwa, ambazo zote ni sehemu ya Uchumi wa Buluu.
Mhe. Salome amemshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati na kueleza kuwa Wizara itaendelea kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha ubora, uwazi na uwajibikaji vinazingatiwa katika kila hatua.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mhandisi Edson Ngabo amewaasa wananchi kutumia miradi ya umeme kama sehemu ya mabadiliko ya maisha kwa kuhakikisha unatumika pia katika shughuli za kiuchumi.
Amesema Serikali inaendelea kuhakikisha miradi ya nishati jadidifu ikiwemo ya jua inakuwa na mchango mkubwa katika gridi ya taifa na nje ya gridi huku moja ya mifano ukiwa ni mradi huo wa umeme jua wa bei ya ruzuku uliozinduliwa pamoja na mradi wa Kishapu wa megawati 150.
Ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kuhusisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya nishati lengo likiwa ni kufikisha megawati 8000 ifikapo 2030.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA , Mhandisi Jones Olotu amesema mradi huo utakaotekelezwa katika mikoa nane kwa miaka miwili ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa nishati (Energy Compact) ambao moja ya azimio lake ni kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi wote ifikapo 2030 na hii ukijumuisha kuunga wateja wapya takriban milioni 8.
Kwa Mkoa wa Mwanza amesema mradi utagusa visiwa 65 kwa gharama ya shilingi bilioni 4.8 ambapo Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 3.3 na pesa iliyobaki wananchi watalipia kwa mfumo wa ruzuku.
Mikoa itakayonufaika na mradi wa kusambaza mifumo ya umeme jua visiwani unaolenga kuweka mifumo 20,000 ya umeme jua katika visiwa 120 ni Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Rukwa, Lindi, Mtwara na Pwani.














