Na Mwandishi Wetu
MRADI wa TACTIC unatekeleza ujenzi wa barabara zenye urefu wa Km 17 kwa kiwango cha lami katika Manispaa ya Geita, mkoani Geita unaotarajiwa kufungua mawasiliano katika Manispaa hiyo.
Ujenzi wa barabara hizo inaelezwa kuwa zitachochea biashara na shughuli nyingine za kijamii katika manispaa hiyo na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi ngazi ya manispaa na mkoa kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bw. Yefred Myenzi ameishukuru Serikali kwa kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi inayogusa moja kwa moja maisha na maslahi ya wananchi.

“Ukiangalia kwa wigo mpana miji inakuwa kwa kasi lakini ile kasi ya kujenga barabara na miundombinu yake ni ndogo, kwa hiyo tunapopata fedha kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu hasa ya barabara, ni fursa kubwa kwa wananchi kwa sababu inaboresha mandhari na muonekano wa mji wetu”, amesema.
Mkurugenzi huyo amesema ujenzi wa barabara hizo unahusisha pia uwekaji wa taa za barabarani hivyo kutoa fursa kwa wananchi kufanya biashara mpaka nyakati za usiku na kuongeza kuwa uwepo wa taa hizo zitaimarisha usalama kwa wananchi wakati wa usiku.
Kwa upande wake, Edward Misalaba Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwatulole amefurahishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mkolani-Mwatulole na kubainisha kuwa utachangamsha mtaa wake na kuwa chachu ya biashara kwa wananchi wake.

Naye, Faraja Magulu ambaye ni Mama Lishe pembezoni mwa barabara hiyo amesema ujio wa mradi huo ni neema kwao kwani utavuta watu wengi hivyo kuongeza wateja na ametoa wito Kwa akina mama wenzake kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara.
Sambamba na ujenzi wa barabara hizo, mradi wa TACTIC katika Manispaa ya Geita unatekeleza mradi mwingine wa ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi ya Mkoa wa Geita ambao upo katika hatua za mwisho za utekelezaji wake.
Akielezea umuhimu wa Stendi hiyo, Bw. Myenzi amesema kuwa kimsingi stendi hiyo kwa manispaa ya Geita ni hitaji ambalo limekuwa ni kilio cha muda mrefu na kuongeza kuwa itawaongezea wigo wa mapato hadi shilingi 2,500,000 kwa siku ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 300 kutoka mapato wanayoyapata sasa ya shilingi 700,000 kwa siku kutokana na stendi inayotumika sasa.


