📌 Watenga maeneo maalumu ya vivuko vya Wananchi na wanyama kuondoa usumbufu wakati ujenzi ukiendelea
*📌Wapongeza Serikali kwa kasi ya ujenzi inayoendelea eneo la kutandaza mabomba ardhini na utoaji ajira kwa wazawa
*📌 Vipande takribani 86,000 kutumika kwenye ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima,Uganda hadi Chongoleani,Tanga.
Na Neema Mbuja, Tanga
Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga haujaathiri shughuli mbalimbali za wananchi kwenye Mkoa na vijiji ambapo bomba hilo linapita.
Hayo yameelezwa leo 18 Julai,2025 wilayani Muheza Mkoa wa Tanga na Msimamizi wa mradi kwenye kipande namba 16 kinachojumuisha uunganishaji wa mabomba na uchomeleaji wake kabla ya utandikaji wa mabomba chini ya ardhi eneo la wilaya ya muheza mkoa wa Tanga Mhandisi Thomas Mhando, wakati alipokuwa akitoa tathmini ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa bomba la EACOP kwa hapa nchini.

‘’ Niwatoe hofu wananchi na watanzania kwa ujumla wananchi wanaendelea na shughuli zao za ujenzi wa Taifa bila kuathiriwa na kazi inayoendelea na wametengewa maeneo maalumu ya kupita na mifugo yao pamoja na madaraja’’ Alisisitiza Mhandisi Mhando.
Amesema kuna jumla ya vijiji 225 kutoka Chongoleani hadi Mtukula Uganda ambavyo mradi unaendelea na utekelezaji wa kazi mbalimbali na bado wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida za kiuchumi na ujenzi wa barabara pia unazingatiwa.
Ameongeza kuwa jumla la vipande takribani 86,000 vya mabomba vitatumika kwa ajili ya usimikaji wa bomba hilo la mafuta ghafi kutoka Uganda mpaka Chongoleani ambapo kila bomba lina ukubwa wa mita 18 kwa ajili ya kusukumia mafuta kuelekea kwenye matenki maalumu ya kuhifadhia mafuta.

Akizungumzia kuhusu ajira za wazawa wakati wa utekelezaji wa mradi wa EACOP Afisa Rasilimali watu kutoka Kampuni ya CPP inayotekeleza mradi kipande namba 16 Bi Draco Kyando amesema kuwa, tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa EACOP wazawa waishio kwenye vijiji ambavyo mradi unapita wamenufaika na ajira na hivyo kuinua uchumi wao.
‘’ Tunaishukuru sana Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya muongozo wa wazawa kwanza (local content) ambapo hadi sasa jumla ya wazawa 369 wamepatiwa ajira katika kipindi cha kota iliyopita ya mwezi wa tatu mpaka wa sita.
Kwa upande wao wananchi walionufaika na ajira kwenye mradi huo wameishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa wananchi wake na kuwapatia ajira na kuongeza kuwa nradi umkuwa mkombozi wa maisha yao na familia zao.

‘’ Niseme tu ukweli mradi huu imekuwa wa mafanikio makubwa sana kwetu si tu kwenye ajira kwa wazawa, bali hata kubadili kabisa maisha ambapo mfano mzuri ni mimi nisingeweza kujenga nyumba kama hii mpaka nakufa kana sio mradi huu wq EACOP’’ Alisema Bwana Abdallah Jumaa mkazi wa kitongoji cha Chanzi.
Kambi namba 16 ni moja ya kambi za ujenzi za mradi wa EACOP ambapo inayohifadhi mabomba yanatumika kwa ajili ya kusukuma mafuta ambayo yanatoka Sojo kuja Muheza kwa ajili ya ujenzi wa mradi.



