* Azindua Baraza la Tatu la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza jipya la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA Consumer Consultative Council – EWURA CCC) kuwa na nidhamu, uzalendo na uwajibikaji katika majukumu yao, ili kuongeza ufanisi wa kazii na kuleta manufaa kwa wananchi.
Akizungumza jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la tatu la EWURA CCC pamoja na mafunzo kwa wajumbe wapya, Mha. Mramba amewahimiza wajumbe hao kufanya kazi kwa ushirikiano na kuweka mbele maslahi ya taifa.
“Ni muhimu kila mjumbe kuwa mfano wa uwajibikaji na uadilifu. Baraza hili lina jukumu kubwa la kusikiliza na kuwasemea watumiaji wa huduma za nishati na maji, hivyo nidhamu na uzalendo ni nguzo kuu za mafanikio.” Amesema Mhandisi Mramba
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa EWURA CCC, Bi. Stella Lupimo, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wajumbe wapya ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, hususan katika kusimamia masuala yanayohusu haki na usalama wa watumiaji wa huduma hizo.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mha. Poline Msuya, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wadau wote wa sekta ya nishati ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora, nafuu na endelevu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji, Bw. Hassan Minga, aliahidi kuwa baraza hilo jipya litajikita zaidi katika kusikiliza changamoto za wananchi na kuzifikisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya utatuzi.
Uzinduzi wa baraza jipya la tatu la EWURA CCC na mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha uwajibikaji, uwazi na uadilifu katika usimamizi wa sekta za nishati na maji, ili kuleta tija na maendeleo kwa jamii.





