Na Mwandishi wa OMH

Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amezindua Mpango Mkakati wa Muda wa Kati wa Benki ya NMB wa mwaka 2026 hadi 2030 (Agenda 2030).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo unaolenga kuboresha utendaji kazi wa benki hiyo, Bw. Mchechu aliupongeza uongozi wa NMB na Bodi ya Wakurugenzi kwa kuifanya benki hiyo kuwa miongoni mwa benki bora zinazochangia kwa kasi ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano, Serikali, inayomiliki asilimia 31.8 ya hisa za NMB, imepata Sh670 bilioni kutokana na uwekezaji wake katika benki hiyo, ambapo kati ya kiasi hicho, Sh224 bilioni ni gawio.

Sanjari na hilo, aliipongeza Benki ya NMB kwa kuoanisha vipaumbele vyake na maono ya Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, hususan katika maeneo ya afya, elimu, ujasiriamali na mazingira.

Katika kusisitiza umuhimu wa mwelekeo huo wa maendeleo, Bw. Mchechu alisema anatamani kuona taasisi zote nchini, ikiwemo za sekta binafsi, zikioanisha mikakati yao na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alitaja Benki ya NMB kuwa mfano wa taasisi inayotekeleza mwelekeo huo kupitia utendaji wake wa kifedha na usimamizi makini wa mikopo.

“Benki ambayo imekuwa ikitoa wastani wa mikopo ya Sh5.6 trilioni kwa mwaka halafu inakuwa na wastani wa mikopo chechefu wa asilimia 2.5 ni kitu cha ajabu sana, hongereni sana NMB,” alisema.

Aidha, aliwataka wateja na wawekezaji kuendelea kuiamini na kupata huduma kutoka Benki ya NMB, akisisitiza kuwa ni sehemu salama kwa kuwekeza fedha zao.