Na Zulfa Mfinanga JamhuriMedia, Arusha
Gazeti la Jamhuri limejizolea sifa kwa namna linavyotunza kumbukumbu za machapisho yake tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011.
Tukio hilo ni sehemu ya Mkutano wa Mabazara Huru ya Habari Afrika (NIMCA), ambao umewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya habari kutoka pembe zote za bara hili.
Akizungumza katika banda la gazeti hilo kwenye maonyesho ya kazi za kihabari yaliyoanza leo jijini Arusha, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Habari-Maelezo ambaye pia ni Msajili wa Magazeti Wakili Evordy Kyando amesema kuwa utunzaji huo wa kumbukumbu ni wa kipekee na unapaswa kuigwa na vyombo vingine vyote vya habari nchini.

“Huu ni mfano wa kuigwa, nawapongeza sana Jamhuri kwa huu ubunifu kwani licha ya dunia kuhamia kwenye mifumo ya kidijitali lakini bado umuhimu wa kutunza taarifa kwa njia ya machapisho halisi haujapotea” amesema Wakili Kyando.
Alieleza kuwa nyaraka hizo ni hazina ya kihistoria ambayo inaweza kusaidia vizazi vijavyo kuelewa mwenendo wa Taifa na matukio ya kihabari kwa undani zaidi.
Amesema kupitia banda hilo amejifunza jambo kubwa na kwamba atahakikisha analifikisha wazo hilo kwa magazeti mengine nchini ili kuiga mfano huo bora wa utunzaji.
“Nikiondoka hapa nitawashawishi wenzangu waliige Jamhuri,” ameahidi.
Kwa upande wao waandaaji wa banda la gazeti la Jamhuri walieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira yao na kwamba wameweka juhudi kubwa kuhakikisha kuwa kila toleo la gazeti lao linatunzwa kwa hali ya juu likiwa limerekodiwa vizuri katika mafaili ya kidijitali na ya karatasi.

Maonyesho hayo yanatoa fursa kwa waandishi wa habari kubadilishana uzoefu na wadau wengine wa habari kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Lakini pia mkutano huo unalenga kujadili mambo mbalimbali ikiwemo kuboresha sheria za habari na mawasiliano barani Afrika, kukuza umahiri wa uandishi wa habari kupitia viwango thabiti pamoja na kuonyesha athari za kazi za habari katika jamii.
Mkutano huo wa siku nne unatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


