Bohari ya Dawa (MSD) imeupokea ujumbe wa wataalamu kutoka Bohari ya Dawa ya Madagascar (SALAMA) kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya, hususan mifumo na mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, alisema kuwa ujio huo ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya afya, kwani mbali na kujifunza pande hizo mbili zitaingia makubaliano ushirikiano.
“Tunafurahi kupokea ugeni kutoka Salama Central Medical Stores ya Madagascar. Ziara hii ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka pande zote mbili. MSD itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za afya ili kuimarisha mifumo ya ugavi wa dawa na kuhakikisha wananchi wanapata dawa salama, bora na kwa wakati,” alisema Tukai.
Tukai amebaisha kwamba MSD itasaini hati ya Makubaliano (MoU) na Bohari ya Dawa ya Madagascar kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu na kiufundi kati ya pande hizo mbili. Makubaliano hayo yanalenga kuwezesha kubadilishana uzoefu, maarifa ya kitaalamu na teknolojia ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi husika.
Aliongeza kuwa kupitia hatua hiyo, MSD na Madagascar zitashirikiana katika masuala ya ununuzi, kubadilishana taarifa na kuimarisha mifumo ya mawasiliano. Ushirikiano huu unatarajiwa kuchangia kuboresha mipango ya pamoja na kuimarisha mahusiano ya muda mrefu kati ya pande hizo mbili.
Naye mwakilishi wa ujumbe huo kutoka Madagascar, ambaye ni Mfamasia Mkuu wa Bohari ya Dawa ya Madagascar (SALAMA), Bi. Soafara Andriamiadamanana, alieleza kuvutiwa na mifumo ya uendeshaji ya MSD, hususan katika maeneo ya maghala ya kisasa na mtandao wa usambazaji wa dawa nchini.
“Tumefurahishwa sana na mifumo ya MSD, hasa usimamizi wa maghala na usambazaji wa dawa. Tumejifunza mbinu muhimu zitakazotusaidia kuboresha utoaji wa huduma za dawa nchini Madagascar,” alisema Andriamiadamanana
Vilevile, ujumbe huo umepata fursa ya kujionea na kujifunza kwa vitendo namna MSD inavyotekeleza majukumu yake manne makuu ambayo ni ununuzi, uhifadhi, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za afya.
Aidha, walielezwa kuhusu mifumo mbalimbali ya kazi inayotumiwa na MSD katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa bora, salama na kwa wakati kwa wananchi.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za MSD kuimarisha uhusiano wa kimataifa na ushirikiano wa kikanda, kwa lengo la pamoja la kuboresha upatikanaji wa dawa salama, bora na kwa wakati kwa wananchi.











