Watendaji wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) wakiongozwa na Meneja wa Masoko ya Kikanda, Nabila Hemed wametembelea Bohari Kuu ya Dawa ya Madagascar (SALAMA) na kuzungumza na uongozi wa bohari hiyo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Claude Eric Ramanantoanina kuhusu njia bora za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo muhimu kwa afya ya binadamu.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Antananarivo Agost 08, 2025, kando ya Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeangazia masuala mbalimbali, ikiwemo namna bora ya kutumia mpango wa pamoja wa nchi za SADC wa kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi ambapo Tanzania kupitia MSD imekasimiwa jukumu hilo kwa niaba ya nchi za SADC.

Bi. Nabila ambaye aliwasilisha mada kuhusu uwezo na ufanisi wa MSD alisema ni muhimu nchi za SADC ikiwemo Madagascar zikautumia mpango huo ipasavyo, kwani pamoja na mambo mengine, unalenga kuzisaidia nchi wanachama kupata bidhaa bora za afya kwa gharama nafuu na kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa hizo ili Kanda ya SADC iweze kujitegemea.
Viongozi hao pia walijadiliana kwa kina kuhusu umuhimu wa kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu yao hususan katika maeneo ya uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Walisema hayo ni maeneo nyeti yanayohitaji ufanisi na ubunifu ili kuepuka changamoto ambazo zinaweza kuzorotesha mfumo wa utoaji wa huduma za afya katika nchi. Hivyo, walisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kupitia taasisi zilizokasimiwa kutekeleza majukumu hayo, kubadilishana uzoefu na taarifa ili ziweze kujikwamua.

Viongozi hao walihitimisha mazungumzo yao kwa MSD kuualika uongozi wa SALAMA kutembelea Tanzania ili kupanua wigo wa majadiliano na kujifunza zaidi.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga na Afisa Sheria Mkuu wa MSD, Bi. Ukundi Domenic.








