Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali imesema inaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini ambapo kwa kipindi cha miaka minne idadi ya vituo vinavyohudumiwa na MSD imeongezeka kutoka 7,095 mwaka 2021/22 hadi kufikia 8,776 mwaka 2024/25.

Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la vituo 1,681 vinavyopokea huduma kupitia kanda 10 za MSD nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ameeleza hayo leo Agosti 15, 2025 katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya sekta ya afya.

Msigwa amesema mafanikio haya ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kupitia MSD, ambayo imekuwa mhimili muhimu wa kusogeza huduma za afya kwa kuhakikisha usambazaji wa dawa na vifaa tiba unafanyika kwa wakati na kwa ufanisi.

Amesema Serikali pia imeongeza thamani ya bidhaa za afya zinazozalishwa na viwanda vya ndani. Kwa mwaka wa fedha 2021/22, bidhaa za thamani ya Sh. bilioni 15.9 zilinunuliwa kutoka kwa wazalishaji wa ndani, na kufikia Sh. bilioni 98.72 mwaka wa fedha 2024/25, hatua iliyopunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kulinda ajira za Watanzania.

Katika kuboresha huduma za kibingwa,Msigwa amesema MSD imenunua na kusambaza vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya Sh. bilioni 429.2 ikiwemo mashine za usingizi, CT-Scan, MRI 3T, Ultrasound na digital X-Ray, vilivyosambazwa katika vituo vya afya nchini.

Amebainisha kuwa Serikali imetoa Sh. bilioni 642.1 kwa MSD kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya, huku mwaka wa fedha 2024/25 pekee ikitolewa Sh. bilioni 196.3 kati ya bajeti ya Sh. bilioni 200, sawa na asilimia 98 ya utekelezaji — rekodi tangu kuanzishwa kwa MSD mwaka 1994.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amesema bohari hiyo itaanzisha mfumo wa kidijitali wa kufuatilia dawa kuanzia kiwandani hadi kwa mgonjwa, ili kuimarisha usalama wa wagonjwa na kuzuia kuingia kwa dawa bandia sokoni.

Tukai amesema mfumo huo utahakikisha dawa zote zinazopita kwenye mnyororo wa MSD ni salama, bora na zenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, hatua inayotarajiwa kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usambazaji wa dawa.

Pamoja na mambo mengine Serikali imesisitiza kuwa dhamira yake ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kujali eneo analoishi, kwa kuendeleza uwekezaji katika MSD na sekta ya afya kwa ujumla, sambamba na kushirikiana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi.