Polisi nchini Canada imethibitisha kuwa msichana mwenye umri wa miaka 18 ndiye aliyefanya shambulio la risasi na kuua watu sita katika shule ya Tumbler Ridge, baada ya kumuua mamake mzazi na kaka yake wa kambo.
Mshambuliaji huyo alijiua baadaye na uchunguzi unaendelea kubaini sababu zilizochochea mauaji hayo ambayo yameelezwa kuwa miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi ya risasi katika historia ya Canada.
Kamanda wa Polisi, Dwayne McDonald, amesema mamlaka bado hazijabaini chanzo cha shambulio hilo la Jumanne. Hata hivyo, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mshambuliaji alikuwa akikabiliwa na matatizo ya afya ya akili.
Polisi wamemtambua mshambuliaji kama Jesse Van Rootselaar, mwanamke aliyebadili jinsia ambaye alizaliwa akiwa mwanaume.
Alikuwa ameacha shule hiyo ya sekondari takriban miaka minne iliyopita. Taarifa hizo zimeibua maswali kuhusu historia yake, mazingira ya kijamii, na iwapo alionyesha dalili za hatari kabla ya tukio.
Serikali ya Canada imetangaza kuwa bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kwa siku saba kote nchini kama ishara ya maombolezo ya kitaifa.
Viongozi wa dunia wametuma salamu za rambirambi na kuonyesha mshikamano na Canada.
Waziri Mkuu Mark Carney amesema tukio hilo limeiacha Canada katika huzuni na mshangao, akisisitiza kuwa taifa linasimama pamoja katika kipindi hiki kigumu.


