ISRAEL bado haijatoa majibu ya uhakika kuhusu mapendekezo mapya ya kusitisha vita kwenye Ukanda wa Gaza ambayo yaliridhiwa siku ya Jumatatu na kundi la Hamas.
Vyanzo vilivyo karibu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu vimeyaambia mashirika kadhaa ya habari kuwa serikali mjini Tel Aviv imedhamiria kuendelea na mipango ya kijeshi ndani ya Gaza ikiwa ni pamoja na kuukamata mji mkubwa zaidi wa Gaza City.
Mpango huo uliotangazwa wiki chache zilizopita ndio umezusha hamkani kimataifa ikihofiwa utazidisha maafa na mateso kwa Wapalestina ambao baada ya miezi 22 ya vita wanakabiliwa na hali mbaya ya kiutu.
Hapo jana, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Qatar, mojawapo ya mataifa mawili ya kiarabu yanayohangaika kutafuta suluhu ya mzozo wa Gaza, ameelezea umuhimu wa kupatikana mkataba wa kusitisha vita haraka, akionya juu ya hatari iliyopo ikiwa hilo litashindikana.
Afisa huyo, Majed al-Ansari, amesema iwapo pendekezo la sasa la kusitisha vita litakwama, mzozo wa Gaza utaongezeka na kufikia viwango visivyoelezeka. Hata hivyo amesema hadi sasa hawajapokea taarifa yoyote kutoka Israel kuhusu pendekezo hilo jipya ya kusitisha vita kwa siku 60.
Pendekezo hilo linajumuisha kuachiwa huru kwa awamu mateka wote wa Israel wanaoshikiliwa Gaza kwa makubaliano ya Israel kuondoa vikosi vyake kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na serikali yake mpaka sasa bado wanapinga sharti la kuondoa wanajeshi Gaza na badala yake wamechagua njia za makabiliano ya kijeshi ili kuongeza mbinyo kwa kundi la Hamas. CHANZO DW
