Na Issa Mwadangala, Songwe

WAZAZI na Walezi mkoani Songwe, wametakiwa kutowalaza watoto wa jinsi tofauti katika chumba kimoja pamoja na ndugu, jamaa au marafiki wanaowatembelea ili kuepuka vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na mahusiano ya kimapenzi.

Wito huo umetolewa na  Afisa Mnadhimu wa Polisi mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Akama Shaaban, wakati akitoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwa wazazi, walezi na watoto waliofika katika Kituo cha Kutambua na Kukuza vipaji vya watoto cha Mwakitwange Toto Center kilichopo Isangu, Mbozi ili kujionea mambo wanayoshiriki watoto hao kituoni hapo.

Alieleza kuwa tafiti zimeonesha kuwa vitendo vya watoto kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi vinaanzia majumbani ambapo watoto wenye jinsi mbili tofauti wanalala chumba kimoja ikiwa ni pamoja na wageni wanaowatembelea.

Aidha ACP Akama alieleza kuwa kuchanganya au kuchukua badaboda tofauti kunapelekea watoto kufanyiwa ukatili pindi waendapo na watokapo skuli na kuwataka wazazi kutofanya hivyo.

“Tafuteni bodaboda mmoja mnaemuamini na kumjua vizuri ili endapo mtoto atafanyiwa ukatili iwe rahisi kumbaini mhusika”, alisema ACP Akama.

Alieleza kuwa watoto wanapoanza vitendo vya mahusiano ya mapenzi wakiwa wadogo hupelekea kutokuwa na mwamko wa masomo na badala ya kujingiza kwenye vitendo hivyo na watu wenye umri mkubwa ambapo ndio chanzo cha ukatili wa kijinsia.

Pamoja na mambo mengine, ACP Akama aliwasisitiza kutosita kutoa taarifa mbalimbali za uhalifu ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Songwe, Mkaguzi wa Polisi, Eletisia Mtweve, aliwataka wanaume kutotelekeza watoto wao kwani kufanya hivyo ni chanzo cha kuwa na watoto wa mitaani na ongezeko la watoto kubakwa na kulawitiwa ili wapate mahitaji yao na wakati mwingine hata kusaidia familia.

Naye Koplo, Gladness Sizya, alisema ni jukumu la kila mzazi au mlezi kuhakikisha anatoa huduma bora kwa mtegemezi wake ili kupunguza vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto katika jamii ili watoto waendelee kuwa salama na watimize malengo ya masomo na maisha yao ya baadae.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo hicho, Rita Kamenya, alilishukuru Jeshi la Polisi mkoani humo kushiriki katika tukio hilo na kutumia fursa hiyo kubainisha huduma wanazozitoa kituoni hapo.

Aidha mkurugenzi huyo, alionesha jinsi alivyofurahishwa na elimu iliyotolewa kituoni hapo na ameahidi kuendelea kushirikiana naa Jeshi hilo hasa kwenye mambo ya usalama na ulinzi wa watoto pindi wawepo kituoni hapo.