Na Dotto Kwilasa, Mpwapwa
Mtetezi wa haki za watu wenye ulemavu Dodoma Maiko Salali amejiweka rasmi kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Ubunge wa Jimbo la Mpwapwa baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika ofisi za chama hicho Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Salali amechukua fomu hiyo Juni 30, 2025, mbele ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya, wanachama na wafuasi waliomsindikiza huku akisisitiza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Mpwapwa kwa uadilifu na uwazi mkubwa endapo atapewa ridhaa ya chama na baadaye wananchi.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Salali amesema anaamini Jimbo la Mpwapwa lina fursa nyingi za maendeleo ambazo zinahitaji kusimamiwa kwa weledi na dira sahihi ya kiuongozi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo ya kweli.
“Kitu kikubwa kwangu ni kuhakikisha kuwa nakuwa daraja kati ya wananchi na serikali, ninayo maono ya kuliletea Jimbo la Mpwapwa mageuzi makubwa katika sekta za elimu, “amesema.

