Na Mwandishi Wetu, Arusha

Mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Imani na mkazi wa Kata ya Osunyai, Jijini Arusha, aitwaye Karim Rahim (9), amefariki dunia kwa madai ya kujinyonga kwa kutumia kipisi cha kitambaa cha dela, baada ya kutazama maudhui ya chaneli ya KIX na kujaribu kuyaiga akiwa nyumbani kwao.

Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa alasiri Julai 20, 2025, ambapo inaelezwa kuwa Karim alimaliza kutazama chaneli hiyo kisha kuingia chumbani akiwa amebeba kashata – vitafunwa ambavyo hupendwa sana na watoto.

Baada ya kuingia chumbani, Karim alifungua dirisha na kuwaona watoto wa jirani, akaanza kuwagawia kashata huku wakiendelea kuzungumza. Dirisha hilo linaelezwa kuwa lilikuwa limefungwa kwa kutumia kipisi cha kitambaa cha dera kutokana na kitasa chake kuwa kimeharibika.

Mama mkubwa wa Karim, Bi. Amina Daudi, amesema kuwa alisikia sauti ya mtoto huyo akiwa anaongea na wenzake, lakini ghafla alipokuwa akimwaga maji ya kudekia, alimuona Karim akiwa amenasa shingoni na kuning’inia pembezoni mwa dirisha.

Amina alipiga yowe, akaingia ndani na kukata kipande cha kitambaa hicho, kisha Karim alikimbizwa katika Hospitali ya Levolosi, lakini madaktari walithibitisha kuwa tayari alikuwa amefariki dunia.

Watoto waliokuwa wakizungumza na Karim walieleza kwa mshangao kuwa walimuona tu “kageukia huko”, ishara kuwa tukio hilo lilitokea kwa ghafla bila wao kuelewa kilichokuwa kinaendelea.

Familia ya Karim imekiri kuwa mtoto huyo alikuwa na tabia ya kutazama chaneli ya KIX kwa muda mrefu, na huenda alijaribu kuiga baadhi ya maudhui yanayoonyeshwa kwenye chaneli hiyo, ambayo hulenga watu wenye umri wa miaka 18 hadi 45, na huhusisha mapigano, mashindano ya nguvu, na matukio ya kihatarishi.

Kwa sasa, tunasubiri taarifa rasmi kutoka kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kuhusu uchunguzi wa kina wa tukio hilo ili kubaini kama kuna maelezo zaidi au tofauti na yaliyotolewa.

Chanzo: GADI TV