Na Manka Damian, JamhuriMedia, Mbeya

MTOTO wa jinsi ya kiume mwenye umri wa siku 14 mkazi wa Mtaa wa Iyela One Kata ya Iyela Jijini Mbeya ameibwa na mtu asiyejulikana muda mfupi mama yake Neema Mkunywa alipotoka kumsindikiza mgeni.

Neema aliyejifungua mtoto huyo wa pekee kwa njia ya upasuaji amesema alifikiwa na mgeni ambaye ni dada yake baada ya maongezi alitoka kumsindikiza umbali wa mita mia tatu na aliporejea hakumkuta mtoto wake ambaye alikuwa amemlaza sebuleni.

Mama wa Mtoto aliyeibiwa

Baada ya kumtafuta bila mafanikio Mmoto wake ikamlazimu kumuuliza mama mwenye wake aitwaye, Aines Lwinga ambaye alisema hakumuona ndipo walitoa taarifa kwa balozi Msaidizi ,Neva Mgode na kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa Gabriel Button ambaye naye alitoa taarifa Polisi.

Taarifa za kuibiwa mtoto huyo zimelipotiwa April 29,2025 kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Iyela One,Gabriel Button na kusema tukio hilo limemsikitisha na ni la kwanza kutokea mtaani kwake huku akiwataka wazazi kuwa makini na familia zao pia kutowaami wageni wanaowatembelea.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika mtaani hapo wananchi wameshiriki kumtafuta mtoto huyo mchanga bila mafanikio wito ukitolewa kwa yeyote anayemshuku mtu aliye na mtoto asiye wa kwake atoe taarifa Polisi au Ofisi yoyote ya Mtendaji Kata.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Matukio ya wizi wa watoto mkoani Mbeya yamekuwa yakijirudia rudia baadhi ya wahalifu wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.