Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Mwanza

Mtoto mchanga wa siku moja mwenye jinsia ya kike ameibiwa baada ya mwanamke mmoja kujitambulisha kuwa ni mke wa mmoja wa mama yake mzazi na kumbeba mtoto baada ya kuruhusiwa hospitalini katika Kata ya Buzuruga wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumzia tukio hilo Februari 9, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa, amesema tukio la wizi wa mtoto mchanga mwenye umri wa siku moja lililotokea Februari 7,2026 majira ya saa 10 jioni huko Buzuruga, Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.

Mutafungwa amesema kuwa Februari 6, 2026, majira ya saa 12 jioni, mwanamke aitwaye Nice Ajunan Renatus (24), mkazi wa mtaa wa Nyasaka Msumbiji, alifika katika Kituo cha Afya Buzuruga kujifungua.

Amesema,mwanamke huyo alijifungua salama mtoto wa jinsia ya kike na kupewa mapumziko katika chumba namba 4 kwenye kituo hicho cha afya.

Akiwa amepumzika ndipo alifika mwanamke jina halijafahamika umri wake unakadiriwa kuwa kati ya miaka 35 au 40 na kujitambulisha kuwa ni mke wa mjomba wake na alifika kwa ajili ya kumuona mzazi huyo ambapo alimpa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumpa chai.

Hivyo siku iiyofuata Februari 7, 2026, majira ya saa 11 jioni, Nice (mama wa mtoto), akiwa na kichanga chake cha siku moja aliruhusiwa kutoka hospitali baada ya hali yake ya kiafya kuimarika.

Hata hivyo wakati anaondoka hospitalini hapo kuelekea nyumbani mwanamke huyo ( mtuhumiwa) alimuomba amsaidie kubeba mtoto ili waelekee wote nyumbani, wakiwa njiani alimpitisha njia za vichochoroni hadi kwenye nyumba ambayo alidai kuwa ni nyumba yake.

“Baada ya kufika katika nyumba moja, alimtaka mzazi huyo kusimama nje kisha mtuhumiwa huyo alizunguka nyuma ya nyumba kwa madai kuwa anachukua funguo lakini cha kushangaza alikaa muda mrefu bila kurudi.

“Familia ya nyumba hiyo ilianza kumtilia mashaka mzazi huyo na walipomuuliza ili kufahamu anasubiri nini ndipo alipoeleza mkasa mzima na kubaini kuwa ameibiwa mtoto mchanga wa siku moja,”amesema Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza hususani akina mama kuchukua tahadhari na kuacha tabia za kuamini watu wasiowafahamu na kuwakabidhi watoto ili wawasaidie badala yake washirikiane ndugu, jamaa na marafiki wanaowafahamu.

“Jeshi la Polisi tunatoa witi kwa yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kupatikana kwa mtoto asisite kuziwasilisha kituo chochote cha Polisi,”amesema Mutafungwa.