Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila imesogea karibu na wananchi kwa kushiriki katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai mwaka huu.

Ushiriki huu unalenga kutoa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi pamoja na kutoa elimu kuhusu namna bora ya kujikinga na magonjwa mbalimbali katika banda namba 16, lililopo Mtaa wa Maonesho Avenue

Huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa magonjwa ya macho na uoni hafifu pamoja na huduma za miwani, uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya masikio, pua na koo, pamoja na uchunguzi wa afya ya uzazi na magonjwa ya kina mama,huduma za radiolojia, matibabu ya magonjwa ya dharura, vipimo vya maabara pamoja na huduma ya ushonaji kwa wanaohitaji huduma hizo.

Hospitali ya Taifa Muhimbili inaendelea kutumia maonesho ya Sabasaba kama jukwaa la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuhamasisha umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yanayoweza kuzuilika mapema.