Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, leo amezindua rasmi mfumo wa dhamana ya forodha wa kikanda (EAC Custom Bond) wakati wa Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Arusha, Tanzania.

Museveni ambaye ameanza rasmi jukumu lake la uenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC, amesema uzinduzi wa mfumo huo ni hatua muhimu katika kuimarisha biashara ya kikanda na kurahisisha usafirishaji wa mizigo ndani ya nchi wanachama.

Mfumo huo wa dhamana ya forodha unalenga kurahisisha taratibu za usafirishaji wa bidhaa mipakani kwa kuwezesha wafanyabiashara kutumia dhamana moja ya kikanda badala ya dhamana tofauti katika kila nchi wanachama.

Kwa mujibu wa viongozi wa jumuiya hiyo, mfumo huo ni sehemu ya miundombinu ya kidijitali inayounganisha taasisi mbalimbali ikiwamo mamlaka za forodha, kampuni za bima, benki, bandari pamoja na mifumo ya ufuatiliaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mfumo huo unafanya kazi sambamba na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mizigo Kikanda (RECTS) ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza muda wa usafirishaji wa mizigo katika ukanda huo kwa hadi asilimia 40 tangu ulipoanza kutumika.

Taarifa za EAC zinaeleza kuwa utekelezaji wa mifumo ya kidijitali katika usafirishaji wa mizigo umewezesha nchi wanachama kuokoa zaidi ya dola za Marekani milioni 250 ambazo hapo awali zilipotea kutokana na ucheleweshaji wa mizigo na udhaifu katika ufuatiliaji wa mapato.

Akizungumza katika mkutano huo, Museveni alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuendelea kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru vinavyokwamisha biashara na kuchelewesha mizigo katika mipaka ya nchi za kanda hiyo.

Amesema ushirikiano wa kikanda katika sekta ya biashara na forodha utaongeza ushindani wa bidhaa za Afrika Mashariki katika soko la kimataifa na kuwapa fursa zaidi wafanyabiashara wa ndani.

Uzinduzi wa mfumo huo umeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha utekelezaji wa Soko la Pamoja na Muungano wa Forodha wa EAC ambao ni nguzo muhimu za ujumuishaji wa kiuchumi wa nchi wanachama.

Hatua hiyo pia itaongeza uwazi katika biashara ya kikanda, kupunguza udanganyifu na kulinda mapato ya serikali huku ikiendelea kuwasaidia wafanyabiashara wanaofuata sheria kufanya shughuli zao kwa urahisi zaidi ndani ya kanda ya Afrika Mashariki.

Aidha Rais Museveni amezindua mkakati wa Saba wa maendeleo ya EAC 2026/2031 unaotekeleza dira ya kimkakati ya juimuiya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo