Tume ya Uchaguzi nchini Uganda imesema Rais Yoweri Museveni ameshinda kwa kishindo katika uchaguzi wa urais wa Uganda. Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Simon Mugenyi Byabakama amesema siku ya Jumamosi.
Matokeo rasmi ya uchaguzi yanaonyesha, Museveni ameshinda muhula wake wa saba kwa kupata asilimia 71.65 ya kura. Kiongozi huyo mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 81 amemshinda mpinzani wake mkuu, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine mwenye umri wa miaka 43 ambaye mepata asilimia 24.72 ya kura. Hata hivyo Bobi Wine, anatarajiwa kuyakataa matokeo hayo rasmi.
Kiongozi huyo wa upinzani amelaani kile alichokielezea kama mchakato usio wa haki wa uchaguzi, ulioharibiwa kutokana na kufungwa kwa mtandao, kuwepo kwa wanajeshi na madai ya kutekwa nyara kwa mawakala wake.
Maafisa wa uchaguzi pia wanakabiliwa na maswali kuhusu kushindwa kwa mashine za utambuzi wa wapiga kura za kibiometriki siku ya Alhamisi, jambo lililosababisha kuchelewa kuanza kwa zoezi la upigaji kura katika maeneo ya mijini ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Kampala ambao ni ngome ya upinzani.
Jumuiya ya waangalizi kutoka Afrika wamekosoa majeshi ya Uganda kwa kuingilia masuala ya uchaguzi wa kiraia nchini Uganda. Katika ripoti zao za awali ambazo waliwasilisha siku ya Jumamosi saa chache kabla ya matokeo ya mwisho kutolewa.
Kiongozi wa Ujumbe wa waangalizi kutoka Umoja wa Afrika, Goodluck Jonathan amesema: “Lazima vyombo vya usalama vijiepushe kutoa maagizo kuhusu masuala ya uchaguzi. Inasikitisha kwamba mkuu wa majeshi mwenyewe ndiye alikuwa wa kwanza kutoa maagizo hayo.”
Waangalizi wanaelezea kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha ghasia katika kipindi cha uchaguzi ni pale watu wanapohisi kunyanyaswa na utawala.
Chama tawala cha Museveni, National Resistance Movement, pia kinaongoza katika wingi wa viti vya bungeni, kulingana na matokeo ya awali ya kura za maeneo bunge ambazo bado zinahesabiwa.
Mapungufu mengine ambayo yameorodheshwa na waangalizi ni madhaifu ya tume ya uchaguzi katika kuendesha elimu ya kiraia, kutojaribisha teknolojia waliyokusudia kutumia ambayo iligoma siku ya uchaguzi na pia tutokuongeza muda baada ya zoezi hilo kuchelewakuanza kwa muda wa zaidi ya saa tatu. Mashine hizo ziliwasilishwa nchini miezi miwili iliyopita na ziligharimu dola milioni 22 za Kimarekani.


