Na Kija Elias, JamhuriMedia, Moshi

Watu watatu wamefariki dunia baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kubomoka kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava, alisema maafa hayo yalitokea eneo la Mbokomu, Wilaya Moshi, usiku wa kuamkia Mei 6, 2025) na kusababisha pia uharibifu wa mali, makazi na miundombinu.

Kwa mujibu wa Mnzava ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama alisema kuwa marehemu wote watatu waliofariki walikuwa wamelala wakati nyumba hiyo ilipowaangukia kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kwamba  majina yao hayajaweza kufahamika mara moja.
Alisema mvua hizo zilisababisha pia kufungwa kwa barabara kuu ya Moshi- Dar es Salaam kufuatia magogo na matope kujaa kwenye daraja lililopo maeneo ya Kiboriloni.

Mbali na vifo hivyo, alisema mvua hiyo pia ilisababisha barabara kuu ya Moshi-Dar es Salaam kutokupitika baada ya magogo makubwa kufunga njia hiyo eneo la Kiboriloni, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

“Tukio linaloendelea kwa sasa ni kuchukua miili ya marehemu ili kwenda kuhifadhiwa kwenye chumba cha maiti wakati maswala mengine ya kushughulikia athari zilizojitokeza zikiendelea”, alisema.
Aidha mkuu huyo wa Wilaya alisema mvua hizo zilizotokea maeneo ya milimani zilisababisha kushusha magogo makubwa ya miti na tope jingi, na hivyo kusababisha mto Kisangiro kufurika na kuifunga barabara hiyo kwa muda mrefu tangu usiku wa manane.

Alifafanua kwamba shughuli za kuondoa magogo na tope eneo hilo zinaendelea kufanywa na Watumishi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakisaidiana na watumishi kutoka vyombo vingine vya usalama.

“Mbali na athari haya kutokea pia kuna nyumba nyingi maeneo ya Kiboriloni Manispaa ya Moshi zimezungukwa na maji,”alisema.

“Kufuatia nyumba hizo kuzngukwa na maji, takribani watu 20 wameponea chupuchupu kusombwa na mafuriko; hali hii imetokana na Mto wa Kisangio ambao unapitia maeneo wanaoishi kufurika”, alisema na kuongeza kufurika kwa mto huo umesbabisha nyumba hizo kuzungukwa na maji.

Diwani wa Kata ya Miebeni Mohamed Mushi, alisema kufuatia mafuriko hayo barabara zote za  kata hiyo zilikuwa hazipitiki kufuatia maji mengi yaliyokuwa yamejaa kwenye madaraja.

Naye Diwani wa Kata ya Mji Mpya Abuu Shayo alisema lisema mvuya za kipindi hiki zimekuwa ni nyingi tofauti na miaka mingine huku akiwataka wananchi waliojenga karibu na maeneo ya mto kuondoka ili w3asiweze kudhurika zaidi.

Kwa upande wake Mrakibu  wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kilimanjaro Jeremiah Mkomagi, alisema jumla ya watu 17 wameokolewa baada ya nyumba zao kuzungukwa na maji.

“Tulipata taarifa majira ya saa 7 za usiku kuhusu maji kuzingira nyumba za wakazi wa eneo hili kufuatia mvua kubwa ilionyesha usiku wa kuamkia leo, watumishi wetu walifika kwa haraka na kuokoa watu ambao walikuwa kwenye hatari kubwa ya kupelekwa na mafuriko”, alisema.

Aliongeza, “Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kuwa baada ya magogo kuziba mto wa Kisangiro, maji hayakuweza kuendelea na mtiririko wake wa kawaida na badala yake yakaelekea kwenye makazi ya watu na kuzunguka nyumba zilizoko karibu na mto huo”.

Mkomagi aliendelea kusema kuwa kufuatia uokoaji uliofanyika hakuna mtu aliyejeruhiwa au kifo kilichotokea eneo hilo la Kiboriloni.