Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mvutano wa kisiasa umeibuka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Mbabala, jijini Dodoma, baada ya baadhi ya makada wa chama hicho kuandamana hadi ofisi za CCM Wilaya wakieleza kutokuwa na imani na diwani mteule wa kata hiyo, Pascazia Mayala, wakidai kushindwa kuleta maendeleo kwa zaidi ya miaka kumi ya uongozi wake.

Mmoja wa wanachama hao, Donarld Mabala, amesema kitendo cha CCM Wilaya kumrejesha Mayala kugombea tena nafasi ya udiwani hakijawatendea haki wanachama, kwani matokeo ya uongozi wake yamekuwa yakikwamisha ustawi wa wananchi wa Mbabala.

“Kata yetu imedumaa kimaendeleo kwa muda mrefu. Tangu achaguliwe hajaleta mradi wowote wa maendeleo na badala yake amekuwa chanzo cha migogoro ya mara kwa mara, ikiwemo migogoro ya ardhi. Hii siyo aina ya uongozi tunaoutaka,” amesema Mabala.

Adela Chiwaligo, mwanachama mwingine wa CCM, ameongeza kuwa licha ya kukosekana kwa chuki za kibinafsi dhidi ya diwani huyo, changamoto kuu ni kushindwa kwake kutatua matatizo ya wananchi na kukwamisha fursa za maendeleo kwa vijana wa eneo hilo.

“Miradi kama ya ujenzi wa barabara ya mzunguko imekuwa ikitupatia fursa ya ajira. Hata hivyo, badala ya kushirikisha vijana wa hapa, yeye amekuwa akiwapa kipaumbele watu anaowataka mwenyewe.

Aidha, amekuwa akitumia lugha za vitisho anapokutana na wananchi badala ya kusikiliza na kutatua matatizo yao,” alisema Chiwaligo.

Hali hiyo imezua mjadala mpana miongoni mwa wanachama, wakitaka chama kuzingatia misingi ya uongozi wa kidemokrasia na utendaji wenye matokeo chanya kwa jamii kabla ya kumpitisha tena diwani huyo katika kura za maoni.

Amepotafutwa kwa maoni yake, Mayala alisema hana cha kusema kwani yeye ni mwana-CCM na uteuzi wake umetokana na maamuzi ya chama.

“Siwezi kutoa kauli yoyote,Mimi ni mtoto wa Chama Cha Mapinduzi na chama ndicho kilichonipitisha,Waende wakamuulize aliyeniteua,nitabaki kuongoza na nitaendelea kutekeleza majukumu yangu,Waache wapige kelele, nitawanyoosha,” amesema Mayala.

Madai haya yanaibua mjadala mpana juu ya uwajibikaji na mizani ya uongozi ndani ya vyama vya siasa nchini, huku wadau wakitoa wito wa kuwepo kwa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya viongozi wa mitaa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo endelevu.