Kardinali Polycarp Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam (Tanzania), alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 katika parokia ya Mwazye, Jimbo Katoliki Sumbawanga, Tanzania.

Kuanzia mwaka 1959 hadi 1964 alipata elimu yake ya sekondari katika seminari ndogo ya Kaengesa. Mwaka 1965 aliingia Seminari Kuu ya Kipalapala kwa miaka mitatu ya falsafa (1965–1967) na miaka minne ya teolojia (1968–1971).

Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre katika Jimbo la Sumbawanga tarehe 20 Juni 1971, na kwa muda wa miaka miwili — kuanzia Juni 1971 hadi Julai 1973 — alikuwa Katibu wa Askofu.

Kuanzia mwaka 1973 hadi 1977 alisoma Teolojia ya Maadili huko Roma katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano (Akademia ya Mtakatifu Alfonsus), ambako alipata shahada ya uzamivu (Udaktari). Baada ya masomo yake, alirudi Tanzania na kufundisha Teolojia ya Maadili katika Seminari Kuu ya Kipalapala kwa muda wa miezi tisa mwaka 1977. Kisha akateuliwa kuwa Gambera wa kwanza wa Seminari Kuu ya Segerea, wadhifa alioutumikia kuanzia mwaka 1978 hadi 1983.

Papa Yohane Paulo II alimteua kuwa Askofu wa Nachingwea tarehe 11 Novemba 1983 na akamweka wakfu tarehe 6 Januari 1984, katika Sikukuu ya Epifania, katika Basilika ya Mtakatifu Petro. Alitawazwa rasmi na kukabidhiwa Jimbo tarehe 19 Februari 1984.

Tarehe 17 Oktoba 1986 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo jipya la Tunduru-Masasi, na alitawazwa tarehe 12 Februari 1987.

Aliteuliwa kuwa Askofu Mwandamizi (Coadjutor) wa Dar-es-Salaam tarehe 22 Januari 1990, alitawazwa rasmi kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu tarehe 22 Julai 1992 kufuatia kustaafu kwa Kardinali Laurean Rugambwa.

Jumapili tarehe 2 Septemba 1990, wakati wa Ziara ya Kitume ya Papa Yohane Paulo II nchini Tanzania, Akiwa Askofu Mwandamizi wa Dar-es-Salaam wakati huo alimkaribisha Papa kwa maneno ya heshima mwanzoni mwa mkutano na mapadre na watawa katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Dar-es-Salaam. Katika kulitambulisha Kanisa la Tanzania kwa Papa, alisisitiza hasa uaminifu, upendo na ari ya kulitekeleza jukumu la uinjilishaji.

Tarehe 12 Aprili 1984 alihutubia Mkutano Mkuu wa Nne wa Kawaida wa Baraza Maalum la Sinodi ya Maaskofu kwa Afrika. Mada ya hotuba yake ilikuwa, “Kukuza Zaidi Imani ya Kikristo katika Maisha ya Kila Siku.”

Kuanzia mwaka 2007 hadi 2009, alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mikutano ya Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar (SECAM).

Alikuwa Mjumbe wa Baraza la Makardinali kwa ajili ya Utafiti wa Masuala ya Kimuundo na Kiuchumi ya Kiti Kitakatifu.

Alishiriki katika Konklave ya Aprili 2005 iliyomchagua Papa Benedikto XVI, na pia katika konklave ya Machi 2013 iliyomchagua Papa Fransisko.

Alifanywa kuwa Kardinali na Mtakatifu Yohane Paulo II katika konsistori ya tarehe 21 Februari 1998, akikabidhiwa Kanisa la Bikira Maria wa La Salette (Nostra Signora de La Salette).

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amefariki dunia tarehe 19 February 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete akiwa na umri wa miaka 82.

Raha ya Milele Umpe Ee Bwana, na Mwanga wa Milele Umwangazie, Apumzike kwa Amani. Amina