Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Kijamii (CCK)David Daud Mwaijojele, amechukua rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo leo Agosti 12, 2025, katika makao makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma, kujiandaa kuwania uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Mwaijojele ameeleza kuwa moja ya vipaumbele vyake vikuu ni kuhakikisha wastaafu wanapata maisha bora baada ya kustaafu, akisisitiza kuwa sera za chama chake zitalenga kuweka mazingira rafiki kwa wastaafu kuishi kwa heshima na kupata usaidizi katika changamoto wanazokumbana nazo.

“Wastaafu wengi huwa na hofu kwa sababu ya changamoto za kiuchumi zinazowakumba baada ya kuondoka kazini,kipaumbele chetu ni kuhakikisha tunawajengea uwezo wanapo staafu ili waishi kwa amani,” amesema Mwaijojele.

Mbali na suala la wastaafu, Mwaijojele ameahidi kuendeleza kilimo cha kisasa huku akisisitiza kuboresha elimu kwa kuongeza ubora wa mitaala na mazingira bora kwa walimu.

Aidha ametoa shukrani kwa INEC kwa kuendesha mchakato wa uchukuaji fomu kwa uwazi na ufanisi hatua ambayo ameitaja kuwa ni mwanzo mzuri kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Mwaijojele atawania nafasi hiyo akiwa na mgombea mwenza Masoud Ali Abdalla, ambaye ameahidi kushirikiana naye kikamilifu katika kutekeleza sera na mikakati ya chama.

Kwa mujibu wa ratiba ya INEC, Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utafanyika Oktoba mwaka huu huku zoezi la uchukuaji fomu likiendelea kwa muda uliopangwa na Tume.