Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Ali Mwalimu,ameahidi kama atakuwa Rais wa Tanzania ataleta neema kwa watanzania pamoja na serikali yake kufanya kazi kwa uadilifu na uwajibikaji ili kumletea maendeleo mwananchi.
Mwalimu ambaye alitinga majira saa 6 mchana katika viunga vya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) akiambatana na mgombea mwenza, Devotha Minja pamoja na wapambe ambao walikuwa wakicheza kwa madoido kupitia matarumbeta na ngoma zikizokuwa zikipigwa.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Salum Mwalimu amesisitiza kuwa moja ya nguvu kuu ya chama chake ni usafi wa rekodi na dhamiri, jambo ambalo limeiwezesha CHAUMMA kujiweka wazi mbele ya Watanzania bila aibu wala woga wowote au deni kwa mtu yeyote.
“Mimi kiongozi msafi, sina deni lolote kwa mtu, sina aibu kwa sababu ya usafi wangu wa dhamiri na matendo,mimi na mgombea mwenza ni wasafi na tunatoa fikra safi, bila mawaa yoyote ambayo yangezuia mustakabali wa taifa letu,” amesema Mwalimu, akisisitiza kuwa msingi wa uongozi bora ni uwazi na uadilifu.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni msingi imara wa kuleta mabadiliko makubwa yanayohitajika kwa taifa.

Licha ya hayo Mgombea hiyo wa CHAUMMA anetaja Kipaumbele cha chama hicho kuwa ni kuinua sauti ya wananchi na kuleta mageuzi na kwamba Kampeni rasmi itazinduliwa Zanzibar, ambapo chama kitaanza kuomba ridhaa kwa Watanzania wote kutuamini ili tuwatumikie.
Pia amewashukuru wananchi wa Dodoma kwa mapokezi makubwa waliyompa, akisema hiyo ni ishara nzuri ya kuonyesha ushujaa wa taifa katika kushirikiana kuleta mabadiliko.
Kuhusu mabadiliko wanayotaka kuleta, mgombea huyo amesema msingi wa mageuzi utaanzia katiba mpya.
“Tutaenda kuanzisha serikali inayolenga haki za watu, na kuwahakikishia uhuru wa kweli bila hiana yoyote,” amesema.

Aidha, amewahakikishia Watanzania kuwa rekodi safi na upya wa chama hicho ni dhamana ya uhuru na maendeleo ya taifa.
“Watanzania watarajie kuona Tanzania yenye neema na maendeleo ambayo Mungu ametupatia,tumekulia maisha ya umaskini, lakini tunayaelewa maisha hayo na tunawapa matumaini kuondokana na hali hiyo,” amesema.
Mwalimu amewataka Watanzania kujiandaa kwa mabadiliko makubwa katika uchaguzi ujao na kuahidi kupambana kwa nguvu zote ili kuleta mustakabali bora kwa taifa.

“Safari hii sio ya mtu mmoja, bali ni ya chama chote na Watanzania wote wanaotaka kuona maendeleo na mabadiliko chanya,” amesema.
Naye mgombea mwenza wa Urais kwa tiketi ya CHAUMMA, Devota Minja, amewahimiza Watanzania kuendelea kuwaamini wanawake na kutoonesha dhihaki kwenye nafasi zao katika siasa na maendeleo ya taifa.
Amesisitiza kuwa wanawake ni nguzo muhimu katika kusukuma agenda za maendeleo hasa katika sekta za afya, elimu, maji, na masuala ya afya ya uzazi.
“Watanzania wanatambua uwezo wa wanawake katika nafasi za uongozi,tumeona wanawake wanaweza kusaidia kuleta mageuzi makubwa hasa kwenye masuala yanayogusa maisha ya kila siku,mimi na mgombea mwenza tutashirikiana kwa dhati kusukuma gurudumu hili kwa maendeleo ya Watanzania,” amesema Minja.







