Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Rukwa

Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linaendelea kufanya uchunguzi wa kina juu ya binti ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne (18) wa shule ya sekondari Nkasi ambaye amejifungua na kumtupa mtoto chooni .

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa Shadrack Masija amesema kuwa mwanafunzi huyo akiwa mjamzito bila ya mtu yeyote kufahamu alijifungua mtoto kisha kumtupa mtoto kwenye choo cha shimo na yeye kwenda shuleni kuendelea na masomo.

Amesema kuwa baada a kitendo hicho watu walisikia sauti za mtoto huyo zikitoka ndani ya choo hicho na taarifa hizo ziliwafikia Polisi ambao walifika eneo la tukio na kumuokoa mtoto huyo ambaye yupo hai.

Amesema kuwa baada uokozi huo mtoto alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.

Kamanda Masija amesema kuwa baada ya mahojiano katika shule hiyo, mwanafunzi huyo alikiri kuhusika na kitendo hicho na kudai kuwa alifanya hivyo bila ya kujitambua na hajui nini kilimfanya amtupe mtoto huyo chooni.

Amesema kuwa baada ya mwanafunzi huyo kukiri alifanyiwa vipimo na kubainika kuwa ni kweli hivyo alikabidhiwa mtoto huyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa wataalamu ambao hawakutaka kuandikwa majina yao, walisema kuwa huenda binti huyo alikumbwa na tatizo la afya ya akiri wakati akijifungua .

Hata hivyo walisema Jeshi la Polisi linaendelea na chunguzi wa tukio hilo na itakabainika alifana kitendo hicho kwa makusudi hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.