Na Allan Kitwe, JamhuriMesia, Tabora
MWANAFUNZI wa kike (jina limehifadhiwa) katika shule ya sekondari ya wasichana Tabora (Tabora girls) Mkoani hapa amejifungua mtoto chooni akiwa shuleni hapo hali iliyoibua sintofahamu kwa uongozi wa shule hiyo.
Hali hiyo imemfanya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Matiko Chacha kufika shuleni hapo na kutoa maagizo kwa Jeshi la Polisi kumsaka kijana aliyempa ujauzito mwanafunzi huyo ili achukuliwe hatua kali za kisheria.
RC ametoa agizo hilo juzi alipofanya ziara ya kushtukiza katika shule hiyo ili kuzungumza na uongozi wa shule na wazazi kufuatia mfululizo wa matukio yaliyoibua sintofahamu katika shule hiyo kongwe hapa nchini.
Alieleza kusikitishwa na hatua ya mwanafunzi huyo kupata ujauzito na kukaa nao kwa miezi 9 bila walimu kugundua suala hilo, hivyo akaagiza hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wote waliohusika na uzembe huo.
Aidha aliagiza kuchunguzwa Daktari aliyemfanyia vipimo mwanafunzo huyo awali na walimu wote waliokaa shuleni hapo zaidi ya miaka10 wahamishwe ili kubadilishiwa mazingira ya kazi kwa kuwa wanafanya kazi kwa mazoea.
‘Mwalimu aliyekaa hapa shuleni kwa miaka 10 au zaidi anafanya kazi kwa mazoea, hafuatilii nidhamu wala mienendo ya wanafunzi, pia haingii akilini kwa mwalimu wa darasa kutojua hali ya wanafunzi wake hususani wa kike’, alisema.
Awali akitoa taarifa ya tukio hilo Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. John Mboya, alieleza kuwa mwanafunzi huyo (jina na taarifa zake zimehifadhiwa) alitoa taarifa ya kuumwa na kupelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete.
Baada ya kupokelewa na kufanyiwa vipimo majibu yalibainisha kuwa amejifungua mtoto hali ambayo iliulazimu uongozi wa Wilaya na Mkoa ukiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa kuunda timu maalum ili kuchunguza hali hiyo na mwenendo mzima wa uendeshaji wa shule hiyo.
Taarifa ya uchunguzi ilibaini kuwa mwanafunzi huyo aliripoti shuleni hapo akiwa na ujauzito lakini cha kushangaza zaidi ni kuwa hakuna mwalimu wala kiongozi yeyote wa shule aligundua hali hiyo hadi kufikia hatua ya kujifungua chooni.
‘Hili linasikitisha sana, vitendo vya wanafunzi kujihusisha na ngono wakiwa shuleni vimekuwa vikipigwa marufuku mara kwa mara, wazazi tunapaswa kushirikiana na walimu kukemea tabia hii’, alisema Dkt Mboya.
Uchunguzi pia ulibaini kuwa hali ya utendaji shuleni hapo imeathiriwa na baadhi ya walimu kukaa kwa muda mrefu katika kituo kimoja cha kazi bila uhamisho hali ambayo husababisha mazoea, kuvuja maadili ya kazi na kutodhibiti nidhamu.
