Wanajeshi watano wa Marekani walijeruhiwa baada ya sajenti wa Jeshi la Marekani kufyatua risasi kwenye kambi moja huko Georgia.

Kwa mujibu wa maafisa wa kijeshi, baada ya sajenti kwa jina Cornelius Radford kuwafyatulia risasi askari wenzake katika kambi ya Fort Stewart, askari waliokuwa eneo la tukio walimvamia na kumnyang’anya silaha.

Tukio hilo lilitokea Jumatano asubuhi. Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya Marekani Carolyn Leavitt, Rais wa Marekani Donald Trump amefahamishwa kuhusu tukio hilo Kwa mujibu wa maafisa wa kijeshi, silaha iliyotumika katika shambulio hilo si ya jeshi la Marekani na uchunguzi unaendelea kubaini jinsi iliingia kwenye kambi hiyo.

Jenerali John Lubas, kamanda wa Kitengo cha 3 cha Wanajeshi wa Jeshi la Marekani, ametangaza hali za wanajeshi waliojeruhiwa kuwa nzuri.

Kulingana na Jenerali Lubas, mshambuliaji huyo alikuwa mwanajeshi kutoka katika ngome hii na hakuwa na historia ya kuwa katika maeneo ya vita. Pia aliwapongeza askari waliompokonya silaha mara moja mshambuliaji huyo na kumkabidhi kwa polisi.

Kwa mujibu wa Jenerali Lubas, shabaha ya shambulizi hilo haijajulikana na mshambuliaji anahojiwa. Fort Stewart iko katika mji wa pwani wa Hinesville, kilomita 386 kutoka Atlanta.