Sekta ya Madini Tanzania imepitia mabadiliko makubwa kutoka enzi za ukoloni hadi sasa. Kabla ya Uhuru, uchimbaji uliendeshwa na wakoloni kwa kiwango kidogo. Baada ya Uhuru mwaka 1961, Serikali ilianza kuimarisha tafiti za jiosayansi na usimamizi wa rasilimali hizo.

Kuanzia miaka ya 1990, mageuzi ya kiuchumi yalifungua milango kwa wawekezaji wa kimataifa na kuongeza uzalishaji. Katika kipindi hicho, mageuzi makubwa yaliendelea kufanyika hususan upande wa Sheria na Sera, ambayo yalipelekea ushiriki mkubwa wa Serikali katika uwekezaji na ukusanyaji wa mapato.

Itakumbukwa kwamba baada ya Uhuru mwaka 1961, Tanzania ilianza rasmi safari ya kujenga mifumo na taasisi za kitaifa za kusimamia rasilimali madini. Serikali ilijenga miundombinu ya utafiti wa jiosayansi kupitia Idara ya Upimaji na Uchoraji Ramani za Jiolojia (GSD), ambayo baadaye ilibadilika kuwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ikiwa na jukumu la upimaji na kuhamasisha uchimbaji mdogo kwa wananchi.

Katika kipindi cha Ujamaa kuanzia miaka ya 1970, kulikuwa na mwelekeo wa umiliki wa serikali kupitia mashirika ya umma likiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), yakilenga kuhakikisha rasilimali madini zinawanufaisha wananchi. Hata hivyo, ukosefu wa mitaji, ujuzi na teknolojia ulidhoofisha ukuaji wa sekta katika kipindi hicho.

Mageuzi makubwa yaliibuka kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa 1990, wakati Tanzania iliporuhusu uwekezaji wa sekta binafsi na makampuni makubwa ya kimataifa katika rasilimali madini. Sheria mpya zilifungua fursa za uchimbaji mkubwa wa dhahabu, na nchi ikawa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika. Pamoja na ukuaji huo, kulijitokeza changamoto za mapato madogo kwa Serikali na migogoro ya kijamii.

Katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imefanya mageuzi ya kina katika Sheria ya Madini Sura 123 na Kanuni zake ili kuongeza usimamizi, uwazi na ushirikiano kwa manufaa ya taifa. Mathalani, mageuzi ya mwaka 2017 yaliyolenga kuhakikisha umiliki wa Serikali kwenye miradi mikubwa na kudhibiti usafirishaji wa madini ghafi, yameweka msingi imara wa maendeleo endelevu ya sekta.

Kupitia juhudi mbalimbali, Sekta ya Madini imeendelea kupiga hatua kubwa. Kwa mfano, ukusanyaji wa maduhuli umeongezeka kutoka shilingi bilioni 623.24 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 753.18 mwaka 2023/2024. Juhudi hizo ziliendelea ambapo kufikia mwezi Juni 2025, Wizara ya Madini ilifanikiwa kukusanya shilingi trilioni 1.071, sawa na asilimia 100.071 ya lengo la mwaka husika.

Sambamba na hapo, Sekta ya Madini imeendelea kuwa mhimili mkubwa wa upatikanaji wa fedha za kigeni. Mwaka 2023, mauzo ya madini nje ya nchi yalifikia Dola za Marekani bilioni 3.55. Kufikia mwezi Septemba 2025 mauzo ya Dhahabu pekee nje ya nchi yamefikia Dola za Marekani bilioni 4.322.4 ambapo Sekta ya Madini inachangia zaidi ya asilimia 56.2 ya mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi. Aidha, kampuni za wazawa zimeendelea kunufaika kwa kiasi kikubwa, ambapo bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.3, sawa na asilimia 92 ya thamani ya manunuzi yote ya migodi, zilitolewa na Watanzania.

Sekta ya Madini imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania, ikiwa na mchango wa asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa kufikia mwaka 2024 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya lengo.

Katika kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa nguzo imara ya uchumi wa taifa, Serikali inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuifanya sekta hii iwe na uchumi jumuishi, ikiwemo kuhakikisha madini adimu na madini mkakati yanaongezwa thamani hapa nchini kabla ya kusafirishwa nje.