Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Simanjiro

Mwenge wa uhuru mwaka 2025 utakagua, kuzindua na kutembelea miradi 51 ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 71.3 katika Mkoa wa Manyara.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameyasema hayo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, wakati akikabidhiwa mwenge wa uhuru na mkuu wa mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi.

Sendiga alisema ukiwa katika mkoa wa Manyara mwenge wa uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 1,197.10 kwenye halmashauri saba za Simanjiro, Kiteto, Babati vijijini, Babati mjini, Mbulu mjini, Mbulu vijijini na Hanang’.

Alisema mwenge wa uhuru unaotarajia kuweka mawe ya msingi katika miradi 11 ya thamani ya Sh9.7 bilioni, kuzindua miradi 16 ya thamani ya Sh5.5 bilioni na kufungua mrad mmoja wa thamani ya Sh98.4 milioni.

Alisema mwenge wa uhuru utakagua na kuona miradi 23 ya thamani ya Sh bilioni 55.9 na nguvu za wananchi Sh milioni 330.

Alieleza kwamba katika fedha hizo Sh71.3 bilioni, serikali kuu imetoa Sh bilioni 62.2 na mamlaka za serikali za mitaa kupitia mapato ya ndani imetoa Sh bilioni 1.9 na wadau wengine Sh bilioni 6.9.

“Nawashukuru na kuwapongeza watu wa mkoa wa Manyara, kwa kuibua, kuanzisha, kuchangia na kuitekeleza miradi hiyo ya maendeleo,” alisema Sendiga.

Mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2025, Ismail Ussi amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni jtokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani.

“Mwaka huu wa 2025 tujitokeze kwa wingi kupiga kura za mgombea wa Rais, wabunge na madiwani ili tuweze kupata maendeleo zaidi kupitia hao,” alisema.