Na Ruja Masewa, JamhuriMedia, Mbeya
Mwenge wa Uhuru unepokelewa kwa shamrashamra kubwa mkoani hapa, huku ukiiangalia miradi ya shilingi Bilioni 30 za Kitanzania.
Mwenge huo ulipokelewa leo Oktoba 13, 2025 katika Viwanja vya Hasanga, Uyole Mbeya, ukitokea Wilaya ya Rungwe, ambapo Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ally Ussi alimkabidhi Mkuu wa wilaya hii Solomon Kitunda,
Akiuongoza Mwenge huo ili Umulike, Ussi ametembelea, kukagua na kuzindua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 30.

Miradi hiyo ni pamoja na Kituo cha Afya cha Isyesye, Mradi wa Maji wa Forest unaotumia chanzo cha Mto Kiwira, Barabara ya Iwambi,, Shule ya Kingereza (English Medium) iliyojengwa na Vijana kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri.
Miradi mingine ni Mradi wa Usafi wa mazingira wa vikundi vya Vijana, Wanawake na Ukarabati wa miundombinu ya shule ya Azimio (Sisimba) ikiwa na Madarasa, Bwalo, na Matundu ya Vyoo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Ussi amewataka Wananchi wa Mbeya kuuenzi Mwenge wa Uhuru kwa kudumisha Amani, kushiriki shughuli za maendeleo, na kuilinda miradi inayotekelezwa na Serikali.

“Mwenge wa Uhuru unamulika Kupambana na Rushwa, Malaria, Lishe duni iwe bora, pamoja na kutokomeza ukimwi kama alama ya matumaini, uzalendo na ushirikiano kwa Wananchi wote”.alisema Ussi.
Aidha Ussi pia alifunga Kongamano la vijana la kitaifa lililoanza Oktoba 10, 2025 jijini hapa na kuwataka vijana kudumisha vipaji walivyo navyo kwa kuwafumdisha wengine, huku akiwaasa Wasishawishiwe kuingia katika uvunjifu wa Amani bali waijenge nchi.
Aliongeza; Hakuna mtu atakayetoka Ulaya au Nchi ya Jirani kuja kuleta Maendeleo isipokuwa wao, hivyo wadumishe Amani, kwa kuweka matumaini, Upendo na Heshima kwa wananchi, kama dhima kuu ya kuwasha mwenge wa uhuru nchini.
Walioupokea Mwenge na Miradi hiyo kwa Shamrashamra, ni pamoja na Rais wa Umoja wa Mabunge duniani (IPU) na Mgombea wa Ubunge Jimbo la Uyole Dk. Tulia Ackson, Viongozi na Wananchi wa makundi mbalimbali, ambapo wamemshukuru Mgombea wa Urais Dk. Samia Sulubu Hassan.

Mwenge huo ambao mwaka huu una Kauli Mbiu “Jitokeze kupiga kura kwa Amani na Utulivu” utazimwa tarehe 14 Oktoba 2025, hapa Mbeya uwanja wa Sokoine na Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia ambapo Viongozi mbalimbali watahudhuria.


