Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini na Mjumbe wa Kamati Kuu, Abeid Mayala amejiondoa kwenye chama na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Mayala amejiunga na CCM wakati wa mkutano wa kampeni za mgombea urais wa chama,Samia Suluhu Hassan kwenye uwanja wa Cheka wilayani Ilala, Dar es Salaam leo Oktoba 22,2025.


Amesema amekuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Ruvuma kwa muda mrefu.
Amesema ameitumikia Chadema kwa miaka 18, lakini baada ya kutafakari kwa kina amebaini ndani ya chama hicho kuna matatizo.


Amesema makada wengi wa Chadema wanaishi maisha ya kunyanyaswa baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa chama hicho, uliomchagua Tundu Lissu kuwa mwenyekiti.


“Uchaguzi mkuu wa Chadema ulimalizika lakini kutokana na kuwa upande wa pili kwa maana ya kumuunga mkono aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe,tumebaki watu wa kunyanyaswa,”amesema

Anasema wakiwa na mkutano wa Kamati Kuu mkoani Mbeya walikubaliana kuingia kwenye uchaguzi,lakini kiongozi mmoja alikataa.
“Nimekuja kuungana na CCM kwa sababu tatu kubwa.mosi nimesoma Ilani yako nikaona unakwenda kuandaa Katiba mpya, hiki ndiyo kilikuwa kilio chetu Cha muda mrefu,”amesema.


“Mama tumekuwa na kilio cha muda mrefu kuhusu Katiba, limenigusa sana,
utakuwa umefanya jambo jema sana,”amesema.


Kuhusu tishio la kuwepo maandamano, amesema hakuna kitu kama hicho na kuwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi Oktoba 29 kwa ajili ya kupiga kura.


“Nikuhakikishie uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba 29,hakuna maandamano,”amesema.
Amesema sababu ya pili amesema amesoma Ilani na kubaini ina sera nzuri ambazo zinatakelezeka.


“Nimesoma sera na kuona ni nzuri, mwenyekiti una uwezo mzuri wa kutuongoza Watanzania,”amesema.
Amesema hata baada ya kifo cha Rais John Magufuli, àmeongoza nchi vizuri.


“Mama baada ya Kifo cha Hayati Magufuli umeupiga mwingi kila mmoja wetu ameona unastahili,”amesema.


Kada huyo mpya amewaomba radhi viongozi wawili wa Chadema, Joseph Mbilinyi (Sugu) na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani,Jacob Boniphace kwa kuondoka bila kuwaaga.


“Niwaombe radhi ndugu zangu Sugu na Boniphace ningewaaga wangeniambia nibaki,,”amesema.