Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Meatu
Watoto 53 kutoka vijiji 16 vinavyozunguka Pori la Akiba la Maswa wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa miguu vifundo , matege na midomo sungura kupitia msaada wa Mwiba Holdings Ltd.
Kampuni ya Mwiba ambayo ni kampuni tanzu ya Fredkin Conservation Fund (FCF) Imewekeza shughuli za Utalii,wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu.
Afisa Uhusiano wa Mwiba Holdings, Mulisu Richard Ngassa, akizungumza na waandushi wa habari wilayani hapa baada ya kukamilika zoezi maalum la utambuzi wa watoto wenye changamoto za ulemavu katika vijiji hivyo alisema kati ya watoto 131 waliobainishwa, 51 wanahitaji mazoezi tiba (physiotherapy).
Alisema watoto 27 watakuwa
wakifuatiliwa kwa mwaka mmoja kabla ya kuanza matibabu na Watoto 53
wanatarajia kufanyiwa upasuaji mwezi huu KAFIKA House, jijini Arusha.

Ngasa alisema mwezi Agosti mwaka jana, watoto 64 walibainishwa kuwa na changamoto za kupatiwa matibabu, ambapo zaidi ya 28 tayari wamefanyiwa upasuaji na kuruhusiwa kurejea majumbani wakiwa na afya njema.
“Bado kuna wengine bado wanaendelea na matibabu na wanatarajiwa kurejea majumbani kwao hivi karibuni wakiwa na afya tele”alisema
Meneja miradi wa Taasisi ya Friedkin Conservation Fund(FCF) Aurelia Mtui alisema kwa sasa, Mwiba Holdings ipo kwenye mazungumzo na watoa huduma wengine wa afya ili kuhakikisha inawafikia wahitaji wengi zaidi, hususan katika huduma ambazo hazitolewi na KAFIKA House kwa sasa.
Mtui alisema huduma hizo zinahusisha matibabu ya viungo mbalimbali (tumor
management), watoto wenye vichwa vikubwa (hydrocephalus) pamoja na changamoto zamgongo wazi (spina bifida).

” Hatua hii inalenga kupanua wigo wa kuwafikia wahitaji na kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata tiba stahiki na tutaendelea kushirikiana na serikali za vijiji,halmashauri na wilaya kusaidia matibabu kwa watoto “alisema
Viongozi wa Halmashauri ya Meatu
Aliyekuwa Mwenyekiti mstaafu Philipo Anthony na Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri hiyo, Bonji Bugeni, wamepongeza msaada unaotolewa na Mwiba Holdings wakisema umeleta faraja
kubwa kwa wazazi na watoto waliokosa uwezo wa kugharamia matibabu.
Anthony ambaye ni mkazi wa kijiji cha Makao ambapo Mwiba imewekeza alisema msaada huo ni ushahidi wa manufaa yanayotokana na uhifadhi wa wanyamapori na mazingira katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake Bugeni ambaye ofisi yake imekuwa katika timu ya utambuzi wa watoto wanaohitaji matibabu alisema Mwiba Holdings wamekuwa na msaada mkubwa kwa jamii.

“Mwiba wamerejesha faraja na matumaini kwa familia na watoto wengi wilayani Meatu kwani licha ya kusaidia matibabu wamekuwa wakitoa ufadhili wa masomo,kusaidia ujenzi vituo vya afya,kituo kupambana na wanyama wakali”alisema
Wazazi watoa shukrani.
Miongoni mwa familia ambazo tayari zimenufaika na matibabu kwa watoto walishukuru Mwiba Holdings kwa msaada huo.
Timotheo Ngassa, mkazi wa Kijiji cha
Sapa, alisema mtoto wake Emmanuel alikuwa amelazwa kwa zaidi ya miezi mitatu bila kufanyiwa upasuaji kutokana na gharama kubwa, lakini kupitia msaada wa Mwiba alifanyiwa bila malipo na sasa anatembea vizuri.
“Kwa niaba ya wazazi wengine tunawashukuru sana Mwiba kwa kugharamia upasuaji wa watoto mwaka jana wamefanya na mwaka huu wanafanya tunawaombea kwa Mungu wakurugenzi wa Mwiba na Friedkin kwa maono haya makubwa kusaidia jamii”alisema.

Emmanuel mtoto aliyefanyiwa upasuaji mwaka jana na amepona aliishukuru Mwiba kwa kumpa nafasi ya kuishi kama watoto wengine wasio na ulemavu.
Mzazi wa mtoto Michael Marcus Mahona, mwenye umri wa miaka 6 kutoka Kijiji
cha Buganza, alisema alihangaika na ulemavu wa miguu uliomnyima uwezo wa kucheza na wenzake na hata kujiamini shuleni.
Mahona alisena , baada ya mtoto wake kupatiwa matibabu kituo cha Kafika House amepona maisha yake yalibadilika na anaweza kucheza,kuhudhuria masomo kwa furaha kama watoto wengine.
Mwiba Holdings Ltd imewekeza Meatu katika Pori la Akiba la Maswa, Makao Ranch na hifadhi ya kijiji cha Mwangudo kwa shughuli za utalii wa picha na hoteli.
