Na John Walter-Babati

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Sillo, ameendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya elimu jimboni humo ambapo leo alitembelea Tarafa ya Bashnet, katika kata za Bashnet na Arri.

Akiwa katika Kata ya Bashnet, Mheshimiwa Sillo alikagua ujenzi wa nyumba ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Walahu, mradi wenye thamani ya shilingi milioni 86.

Katika ziara hiyo, Sillo amesema ataendelea kuhakikisha mazingira ya elimu pamoja na miundombinu mingine ya elimu inaboreshwa ili kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Walahu, Agatha Masauda, amesema nyumba hiyo imekamilika kwa asilimia 98 na kuishukuru Serikali kwa jitihada kubwa zinazochukuliwa kuboresha mazingira ya walimu, jambo linaloongeza morali ya kazi na kuwavutia walimu kufanya kazi katika maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bashnet, Jovitha Mandoo, amemshukuru Mbunge Sillo kwa kupambania maslahi ya walimu na kuhakikisha miradi ya elimu inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Ziara ya Naibu Spika pia ilimfikisha katika Shule ya Msingi Arritsaayo, Kata ya Arri, ambako alikagua ujenzi wa madarasa matatu pamoja na matundu sita ya vyoo.

Katika mradi huo, Serikali Kuu ilitoa shilingi milioni 157.7 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu ya elimu ya msingi, madarasa mawili ya elimu ya awali pamoja na matundu 12 ya vyoo.

Kwa sasa, madarasa yote matano yapo katika hatua ya lenta huku ujenzi wa vyoo ukiwa katika hatua ya awali. Mradi huo unatarajiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi wa madarasa ya awali na msingi pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mheshimiwa Sillo amepongeza uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambao umewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo, hususan katika sekta ya elimu.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Arritsaayo, Anna Aweda, ameeleza kuwa ifikapo Januari 28, 2026, madarasa yote matano yatakuwa yamekamilika.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkurugenzi wa Taasisi ya Karimu Foundation Tanzania, Shau Erro, ambao ni wafadhili wa mradi huo, aliyesema kuwa fedha za ukamilishaji zipo tayari na mradi utakuwa umekamilika ifikapo tarehe hiyo.

Aidha, Shau Erro ameahidi kuendelea kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maji, afya na elimu katika kata za Arri na Dabil.

Diwani wa Kata ya Arri, Paulo Masong, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo nyingi na kueleza kuwa haijawahi kutokea kata hiyo kupokea kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya mradi mmoja wa elimu katika shule moja, hatua aliyoitaja kuwa ya kihistoria na yenye tija kubwa kwa maendeleo ya elimu katika eneo hilo.