Naibu Waziri wa viwanda na biashara, Mheshimiwa Dennis Londo ametembelea ofisi za tume ya ushindani nchini (Fair Competition Commission– FCC) ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kulinda ushindani wa haki nchini.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Londo alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa tume hiyo ambapo aliwasihi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo mkubwa ili kuhakikisha maslahi mapana ya taifa yanalindwa.
Akizungumza na watumishi hao, Mheshimiwa Londo alisisitiza kuwa tume ya ushindani ina nafasi muhimu katika kuhakikisha soko linakuwa na ushindani wa haki unaolinda walaji pamoja na kukuza mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara.
“Ni muhimu kila mtumishi kutambua wajibu wake katika kulinda uchumi wa nchi kwa kuhakikisha kuna ushindani wa haki sokoni. Tekelezeni majukumu yenu kwa uzalendo na weledi ili kuendelea kujenga imani kwa wananchi na wadau wa biashara,” alisema Mheshimiwa Londo.
Aidha, alieleza kuwa serikali itaendelea kuipa kipaumbele taasisi hiyo kwa kuimarisha mifumo ya utendaji kazi ili iweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika mazingira ya biashara yanayobadilika kwa kasi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa tume ya ushindani, Bi Khadija Ngasongwa, alimshukuru Naibu Waziri Londo kwa ziara hiyo na kueleza kuwa imekuwa chachu ya kuongeza morali kwa watumishi wa tume hiyo.
Bi Ngasongwa alisema tume hiyo itaendelea kusimamia sheria za ushindani kwa kuhakikisha kunakuwepo mazingira ya biashara yenye usawa na yanayolinda maslahi ya walaji pamoja na wafanyabiashara wanaofuata taratibu.
Aliongeza kuwa tume hiyo imejipanga kuimarisha ufuatiliaji wa masoko pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa ushindani wa haki katika kukuza uchumi wa taifa.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuhakikisha taasisi zilizo chini ya wizara ya viwanda na biashara zinafanya kazi kwa ufanisi katika kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya biashara na viwanda nchini.











