Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Babati

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, Regina Ndege, amekabidhi futari na daku kwa waumini wa kiislamu kwa Madrasa ya Mahad Al Hayaat Islamiya na Msikiti wa Masjid Noor Babati Mjini.

Msaada huo wa Naibu Waziri Ndege umejumuisha vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, maharage, mafuta ya kupikia, tambi, chumvi na juice.

Pia Naibu Waziri Ndege amekabidhi fedha taslimu shilingi milioni moja kwa ajili ya ununuzi wa zulia la msikiti na shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa jiko la kupikia katika madrasa hiyo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Naibu Waziri Ndege amesisitiza umuhimu wa kulinda amani ya nchi na kuwataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri na kuombea amani ya Tanzania pamoja na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tuendelee kuiombea Tanzania kwani hatuna nchi nyingine zaidi ya nchi yetu nzuri ya Tanzania na endapo kukitokea vurugu au machafuko hatuna sehemu nyingine ya kukimbilia,” amesema Naibu Waziri Ndege.

Kwa upande wao, viongozi wa dini wamemshukuru Naibu Waziri kwa msaada huo wakisema umeleta faraja kwa walimu na wanafunzi wa madrasa hiyo, huku wakiahidi kuendelea kumuombea ili Mungu ambariki na kumfanikisha katika huduma yake kwa jamii.

Wameahidi kuendelea kuombea amani ya nchi na kuwaombea viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ili waongoze kwa hekima, busara huku wakimtanguliza Mungu katika maamuzi yao.