Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mirerani
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya amewaongoza maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Manyara na Arusha kwenye maziko ya kiongozi wa kimila Mshili Justin Abraham Ngumee aliyefariki dunia kwa kugongwa na gari na kuzikwa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.
Kwenye maziko hayo Ole Millya ameongozana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Ormemei Laizer, DAS Simanjiro, Warda Abeid Maulid, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kaleiya Melita Mollel, DED Simanjiro Gracian Max Makota, mbunge mstaafu Christopher Ole Sendeka, viongozi wa Serikali, CCM, Madiwani na maelfu ya watu.
Akizungumza kwenye maziko hayo Ole Millya ametoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki kwa kuondokewa na mpendwa wao ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa katika eneo hilo.

“Tukubali tuu kuwa kila mmoja ananamna yake ya kuhitikisha siku zake duniani na hii ajali iliyochukua maisha yake kwa kugongwa na gari imekuwa sababu tuu ya Ngumee kuondoka hapa duniani,” amesema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Ormemei Laizer amesema wanasiasa wengi wamepitia kwenye mikono ya Ngumee kwani alikuwa kiongozi mwenye kujitoa kila wakati.
“Ngumee alikuwa kiongozi wa kimila hata kabla ya kifo chake asubuhi kulitokea tetemeko kubwa la ardhi ambapo wazee wa kimila wakasema hili tetemeko lazima liondoke na mtu mkubwa ndiyo ikawa hivyo,” amesema Kiria.
DAS Simanjiro Warda Abeid Maulid amesema kilichobaki ni kumuombea kwa Mungu ili apumzike kwa amani kwani ameshamaliza safari yake hapa duniani.
“Tunashukuru Mungu kwa kila jambo kwani yeye ndiye mpangaji wa kila jambo na sisi ni waja wake tuu jina lake lihimidiwe,” amesema DAS Warda.
Mbunge mstaafu wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema msiba wa Ngumee umekuwa gundi ya kuunganisha jamii ya eneo hilo kwa kujitokeza kwa wingi.
“Baba mchungaji ukiangalia umati uliojitokeza kwenye maziko ya Ngumee ni maelfu ya watu wamekusanyika pamoja bila kujali Itikadi ya vyama, kabila, dini au tabaka,” amesema Ole Sendeka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kaleiya Melita Mollel amesema ameshiriki kutoa pole na faraja kwa ndugu, jamaa na marafiki wa mshili Ngumee.

Afisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO) Isack Mgaya amesema kipindi cha uhai wake Ngumee walifanya wote kazi akiwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Tanesco.
Mwenyekiti mstaafu wa UVCCM Mkoa wa Manyara, Mosses Komba ameeleza kwamba Ngumee ni kiongozi ambaye alikuwa anafikika kiurahisi kwani hakujitenga na jamii.
Mkazi mwingine Jafari Matimbwa amesema Ngumee alikuwa rafiki wa kila mtu kwani alikuwa anajitoa kwa kila namna na kuacha pigo kwa jamii ya eneo hilo.
Mkazi mwingine Kaanael Minja (Mama Lisa) amesema Ngumee alikuwa anapenda haki hata akipita barabara akimkuta mwanafunzi amevaa sare ya shule ya msingi au sekondari lazima ampeleke shule.
Mkazi mwingine Athumani Ally amesema kutokana na ushawishi aliokuwa nao Ngumee kipindi cha uhai wake, hata wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani walikuwa wanataka awe upande wao ili washinde nafasi hizo.

