Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia Manyara

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Regina Ndege amewataka askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama wa mkoa wa Manyara, kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi ili wajiongezee kipato badala ya kutegemea mishahara pekee.

Naibu Waziri Ndege ameeleza hayo mjini Babati kwenye siku ya askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama mkoa wa Manyara wenye kauli mbiu ya nidhamu, haki, weledi, na uadilifu, msingi wa mafanikio yao.

‎Naibu Waziri Ndege akizungumza wakati akifungua mafunzo ya uwezeshaji, kuongeza ufanisi, kuimarisha uongozi na kujenga uchumi kwa wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama mkoa wa Manyara, amewaasa wajinyanyue kiuchumi.

“Ninawahimiza askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama mkoa wa Manyara kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi kama wanawake wengine ili kuongeza kipato badala ya kutegemea mishahara pekee,” amesema Naibu Waziri Ndege.

Ameeleza kwamba ni muhimu askari wanawake hao kufahamu mipango na mikakati ya kujiinua kiuchumi kihalali kwa sababu kutegemea mishahara pekee siyo vyema kwani haitoshelezi mahitaji ya kila siku.

‎”Nawashauri muache kuingia kwenye mikopo umiza na kandamizi ambayo inalazimisha kuacha kadi za ATM ila kuweni wabunifu wa kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizoeuhusiwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan” amesema Naibu Waziri Ndege.

Amewahimiza askari wanawake hao wa mkoa wa Manyara kuendelea kushirikiana na jamii katika kujenga ulinzi na usalama, mtandao imara na kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.

Mwenyekiti wa mtandao wa polisi wanawake mkoa wa Manyara, Mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP) Christina Mkonongo ameeleza kuwa umoja wa askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama mkoa wa Manyara umekuwa chachu ya ushirikiano wa kiutendaji wa kila siku katika matendo ya huruma kwa jamii.

“Mheshimiwa Naibu Waziri tunashukuru kwa kuja kwako kwani umetujengea uwezo zaidi kupitia nasaha zako na sisi askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama wa mkoa wa Manyara tunaahidi kuteketeza hayo,” amesema SSP Mkonongo.

‎Mkuu wa polisi wilaya (OCD) ya Babati, mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP) Ernesta Mwambinga amesema lengo lao kuu ni kujengea uwezo askari wa kike mkoani humo katika nyanja za kiuchumi, kiafya na kuelewa masuala mbalimbali ya mahusiano.

‎”Tukiangalia dunia ilivyo sasa, sera ya nchi inatutaka kujenga uchumi kuanzia mtu mmoja mmoja na askari kama wanawake wengine wanahitaji kuimarisha uchumi na kujua mipango ya utunzaji wa fedha,” amesema SSP Mwambinga.

‎Mkuu huyo wa polisi wa wilaya ya Babati ameeleza kwamba wanawake wanapokuwa katika hali nzuri ya kiuchumi wakiwa na kifedha wataweza pia kuihudumia jamii kwa weledi na usafi.

‎Mwenyekiti wa mtandao wa askari wanawake wa Magereza mkoa wa Manyara, mrakibu mwandamizi wa Magereza (SSP) Elizabeth Morembwa amesema mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za kurekebisha tabia za wafungwa.

‎SSP Morembwa amesema kiutendaji itasaidia katika kujenga uwezo wa kujiamini kwa watumishi na kutekeleza majukumu yao katika kazi ya kuwarekebisha wafungwa ili wanapotoka waweze kuwa raia wema.