Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtama na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Moses Nnauye, amesema Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kiongozi jasiri aliyelivusha taifa katika kipindi kigumu kilichogubikwa na changamoto za kiafya na kiuchumi, baada ya kurithi uongozi mwaka 2021 kufuatia kifo cha Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Mashujaa, Moshi mkoani Kilimanjaro, Nape alisema Rais Samia alikabidhiwa taifa wakati likiwa katika msiba mkubwa, huku pia likikumbwa na athari za janga la kimataifa la COVID-19, pamoja na kuyumba kwa uchumi.

“Mama huyu alipokea kijiti cha uongozi wakati taifa likiwa gizani — tumepoteza rais wetu, uchumi umeyumba, na ugonjwa wa COVID-19 ulikuwa tishio kwa maisha ya Watanzania. Lakini hakutetereka. Alianza kazi mara moja, akaimarisha huduma za afya, akatafuta dawa, vifaa tiba, na kuimarisha mshikamano wa kitaifa,” alisema Nape.

Alieleza kuwa kwa hatua hizo, Rais Samia aliirejesha nchi kwenye utulivu, akapunguza kwa kiasi kikubwa athari za ugonjwa huo, na kuweka msingi thabiti wa uimarishaji wa uchumi.

“Huu ni uongozi wa vitendo. Badala ya kulalamika, Rais Samia alichukua hatua. Ameiongoza nchi kwa busara, ametoa matumaini mapya kwa wananchi, na leo tunaona matokeo ya uamuzi wake wa kisera na kiutendaji,” aliongeza Nape.

Kwa mujibu wa takwimu alizozitoa, mapato ya serikali yameongezeka kutoka TSh trilioni 18 mwaka 2021 hadi kufikia trilioni 32 mwaka 2025, jambo linalothibitisha kwamba serikali ya awamu ya sita imesimamia kwa mafanikio ukusanyaji wa mapato na kupambana na mianya ya upotevu wa fedha.

“Kama kuna mtu anahitaji ushahidi wa kazi ya Rais Samia, aangalie hizi takwimu. Toka trilioni 18 hadi 32 ndani ya miaka minne. Huu siyo uongozi wa porojo, bali wa utekelezaji. Ndiyo maana CCM imemteua tena kugombea urais. Ameonesha uwezo wa kweli kuongoza taifa hili,” alisema.

Akigusia suala la rushwa, Nape alisema mafanikio hayo ya mapato hayawezekani pasipo uongozi thabiti na wa uadilifu. Alisisitiza kuwa Rais Samia amefunga mianya yote ya upotevu wa fedha kama vile mtu anayeziba ndoo iliyokuwa na matundu.

“Kama ndoo ina matundu, huwezi kujaza maji. Lakini mama huyu ameziba matundu hayo. Amepambana na rushwa na kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo kwa maendeleo ya wananchi,” alisisitiza Nape.

Katika hatua ya kuhitimisha hotuba yake, Nape aliwaomba wananchi wa Moshi na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, na kumpigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuliongoza taifa kwa ufanisi na maono ya maendeleo.

“Kama tungekuwa na serikali ya wala rushwa, tusingeweza kufikia makusanyo ya trilioni 32. Hivyo, ndugu zangu, tusipoteze muda kwa maneno ya wapinzani. Oktoba 29, twendeni tukatie tiki kishindo. Tumchague mama wa kazi, mama wa matumaini, Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alihitimisha.