WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi ametoa wito kwa Nchi za Afrika kuungana kwa pamoja katika kutekeleza mikakati na mipango ya kuendeleza matumizi bora ya Nishati, ili kuokoa upotevu wa Nishati pamoja na fedha ambazo zingetumika kwa uwekezaji usiohitajika.
Mhe.Ndejembi ametoa wito huo leo Desemba 10, 2025 wakati akihutubia Kongamano la Nishati la Umoja wa Nchi za Afrika (AU) katika Makao Makuu ya Umoja huo Addis Ababa nchini Ethiopia.
“Nchi za Afrika zinapokutana hapa kama wadau wa sekta ya Nishati ni lazima tuungane kwa pamoja katika kutekeleza mipango yetu kwa ajili ya Afrika yetu kwani Serikali ya Tanzania ipo tayari kufanya kazi na Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo na Wadau wote katika kuhakikisha tunapiga hatua kubwa ya kiuchumi na kijamii,” Amesema Mhe Ndejembi.

Aidha Mhe Waziri Ndejembi ameshiriki mjadala wa Mawaziri wa Nishati wa Nchi za Afrika ambapo alitoa taarifa ya hatua kubwa iliyopigwa na Tanzania katika kusimamia ufanisi wa Nishati pamoja na matumizi ya Nishati safi ya kupikia.
Mhe. Ndejembi ameeleza kuwa Tanzania tayari imeshazindua na kutekeleza mkakati wa Taifa wa miaka 10 wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia (2024-2034), sambamba na mkakati wa Mawasiliano na kuandaa mpango kazi wa kutekeleza mikakati hiyo ili kuufikia umma wa Watanzania.
” Nchini Tanzania hadi kufikia Novemba 2025 tayari asilimia 23.2 ya wanachi wanatumia Nishati safi ya kupikia ikilinganishwa na asilimia 6.9 ya mwaka 2021, hivyo kama Taifa tumepiga hatua kubwa na ni matarajio yetu tutaongeza idadi kubwa zaidi ya watumiaji wa nishati safi,” Amesema Mhe Ndejembi.
Katika ziara hiyo Mhe Waziri Ndejembi ameambatana na Kamishna wa Umeme na Nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga.






