Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Darves Salaam
Leo tarehe 22 Agosti 2025, Monalisa Joseph Ndala, mwanachama wa ACT-Wazalendo na Katibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo (Mkoa wa Dar es Salaam) ambaye pia ni Naibu Waziri Kivuli wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, amewasilisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa akipinga mchakato wa kumpitisha Luhaga Mpina kuwa mgombea urais wa chama hicho.
Ndala ameeleza kuwa mchakato huo umevunja Katiba ya chama, kanuni za kudumu pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Amesema hatua yake ya kuwasilisha malalamiko hayo imetokana na majibu ya chama yaliyotumwa kwa Msajili na kusainiwa na Katibu Mkuu, ambapo amedai chama kimeshindwa kujinasua kwenye uvunjifu wa vifungu mbalimbali vya Katiba, ikiwemo Ibara ya 11(e) inayotoa haki kwa kila mwanachama kuchagua na kuchaguliwa kulingana na masharti ya chama.
Ndala amesema Katibu Mkuu wa chama amepuuzia Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa chama za mwaka 2015, hususan kanuni namba 16(4)(i), (iii) na (iv) zinazomtaka mgombea wa urais awe mwanachama kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya mwisho wa uteuzi, awe ametangaza mali na vyanzo vyake kabla ya uteuzi, na kuthibitisha kuelewa na kusimamia itikadi na sera za chama.
Aidha, ameeleza kuwa Katibu Mkuu pia amepuuza kanuni 4(8)(a) inayomtaka mwanachama awe ndani ya chama si chini ya siku saba kabla ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi. Kwa mujibu wa Ndala, Mpina alipaswa kuwa mwanachama mapema zaidi, badala ya kujiunga na chama Julai 28, 2025 baada ya kuondolewa kwenye mchakato wa CCM.
Ndala amesisitiza kuwa hatua hiyo imefanya chama kuonekana kama hakina kanuni za uchaguzi, jambo linaloacha mianya ya chaguzi kuendeshwa kiholela. Amesema Mkutano Mkuu wa mwaka 2024, ambao yeye alikuwa mjumbe, haujafuta kanuni hizo za kudumu, hivyo bado ndizo zinazopaswa kutumika.
Amebainisha pia kuwa Katibu Mkuu ameingiza hoja kwamba Kamati Kuu iliandaa mwongozo wa kumpitisha Mpina, lakini kwa mujibu wa Katiba na kanuni, miongozo haiwezi kubatilisha nyaraka hizo kuu. Ameeleza kuwa ujio wa Mpina ulitokea nje ya mchakato rasmi wa uchaguzi ulioanza Januari 15 na kumalizika Mei 25, 2025, ambapo ni Dorothy Semu na Aaron Kalikawe pekee waliokuwa wamejitokeza kugombea.
Ndala amesema kitendo cha kumuingiza Mpina moja kwa moja kwenye kinyang’anyiro kilipelekea vurugu za kisiasa, kwani wajumbe wa Mkutano Mkuu walimshuhudia akiwasilishwa kama mgombea pamoja na Kalikawe, huku Dorothy Semu akilazimishwa kujiondoa licha ya maandalizi aliyokuwa amefanyiwa na chama. Amehoji namna Mpina alivyoweza kujaza fomu na kupitishwa, huku akieleza kuwa majibu yaliyotolewa na Katibu Mkuu kwa Msajili hayakutoa ufafanuzi wa msingi.

Kwa mujibu wa Ndala, licha ya changamoto na gharama za kusimama dhidi ya kile alichokiita uvunjifu wa demokrasia, ameamua kuwa daraja la kulinda kanuni na taratibu za chama. Amesema baadhi ya watu na taasisi wanamtaka Mpina kuwa mgombea kwa maslahi ya kisiasa, lakini ukweli ni kwamba hakufuata taratibu na hivyo anakosa sifa.
Aidha, Ndala ameeleza kuwa amepokea wito wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kufika Agosti 23, 2025 kwa ajili ya kusikilizwa pamoja na upande wa chama. Amesema atahudhuria kikao hicho akiwa na mawakili wake kwa ajili ya kutetea hoja zake.