Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es SalaM

KAMPUNI ya Ndege ya (ATCL), imeendelea kutanua wigo wa safari zake na sasa iko katika mchakato wa kutafuta vibali vya kuanza safari za kutua mji wa Lagos Nigeria, Accra Ghana, Ivory Coast na Dakar Senegal.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mhandisi Peter Ulanga, wakati akizungumzia mafanikio ya shirika hilo ndani ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema hivi kari walianzisha safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na mji wa Kinshansa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hatua inayolenga kupanua mtandao wake wa safari barani Afrika.

Ndege za kampuni hiyo pia zinafanya safarai zake mji wa Lubumbashi DRC na kwa sasa ndege hizo zinafanya safari kwenye vituo 14 ndani ya nchi, vituo 10 Afrika na vitatu nje ya Afrika.

Ulanga alisema wakifanikisha mpango wa ruti hizo mpya ATCL itakuwa ni moja ya kampuni za ndege zinazounganisha Afrika Magharibi, Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika .

Alisema Novemba mwaka jana walirudisha safari ya moja kwa Joharnesburg Afrika Kusini ambayo ilikuwa imesimama kwa muda na mwezi wanne walianza kwenda Kinshansa DRC na wako kwenye maandalizi ya mwisho kwenda Lagos Nigeria kabla ya mwezi Julai.

“Na tutakuwa tunawapeleka abiria wetu kwenye destination zetu za Dubai, Mumbai India na China na hii mipango yote ni kwasababu tuna ndege nyingi ndiyo maana tunakuwa na shauku ya kwenda safari nyingi zaidi nandefu na usalama ni kipaumbele chetu ,” alisema

“Nilipoteuliwa moja ya jukumu nililosisitiziwa ni kuhakikisha safari zinakuwa salama na safari za uhakika na kuondoa malalamiko ya kuchelewesha au kuahirisha safari niliambiwa tutoe gharama nafuu ili watanzania wengi wamudu kupanda ndege na yote hayo naendelea kuyafanyia kazi,” alisema.

Alisema jukumu lingine alilopewa ni kuhakikisha watanzania wanakuwa na imani na shirika lao na kutumia ndege zake kwenye safari zao za kila siku na kuhakikisha wanaopanda ndege hizo wanajisikia fahari kuzitumia kwa huduma bora wanazopewa ndani ya ndege.

“Tunapima delay ya ndege kila siku ili kama kuna ucheleweshaji umetokea leo tuufanyie kazi usijirudie kesho na miezi minne iliyopita tumefanikiwa kupunguza delay kutoka asilimia 80 mpaka kufikia asilimia 10 kwa hiyo watanzania wasiwe na wasiwasi tena na ndege zao,” alisema.

Alisema miaka minne iliyopita serikali ya awamu ya sita ilifanya uwekezaji mkubwa kwa kuipa kampuni ndege saba kati ya hizo ndege mbili za 737 Max ambazo zinaweza kwenda safari ndefu za masafa ya saa nane kwenye mataifa mbalimbali duniani.

Alisema miongoni mwa ndege hizo mpya ni Dream Liner ambayo inauwezo wa kufanya safari za masafa marefu ya saa nane hadi 12 ambayo imeiongezea uwezo kampuni kwenda masafa marefu zaidi.

“Pia tumepokea ndege ya mizigo yenye uwezo wa kubeba hadi tani 54 kwa wakati mmoja ina tupa uwezo wa kwenda Dubai China na maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba dhima ya kukuza biashara inaongezeka siku hadi siku,” alisema

Alisema ndani ya miaka minne serikali ya awamu ya sita imefanya uwekezaji mkubwa ATCL ambao umeiwezesha kampuni hiyo kutoa huduma bora na kuingiza dola za Marekani milioni 375 na kwamba kwa kadri inavyozidi kwenda safari nyingi wataweza kuwa miongoni mwa kampuni zinazoingiza fedha nyingi za kigeni

Alisema wamefanikiwa kuimarisha ujuzi wa wahandisi wa ndege kwani ndio wanatengeneza ndege za kampuni hiyo na kwamba pale wanapohitaji msaada wanaomba wataalamu wa kigeni kuja kusaidia na mkakati wa kampuni ni kuongeza wahandisi wa ndege wengi zaidi.

“Wakati wa UVICO tulipata shida ya kupata vifaa vya kukarabati ndege na si kwa Tanzania tu shida kama hiyo iliyakumba mashirika mengi duniani na sisi ATCL tuliathirika zaidi na tulichukua hatua ya kutengeneza ndege zetu wenyewe na zote zinafanyakazi vizuri,” alisema