Na Magrethy Katengu,JamhuriMedia
Dar es Salaam

Mgombea Ubunge Jimbo la Mbagala kupitia Chama Cha Wakulima(AAFP) Ndonge Said Ndonge amesema kwamba endapo Wananchi watampa ridhaa ya kuwa Mbunge wao,atashughulikia kero zote za Mbagala ikiwemo mradi wa fremu anaodai kuwa umejengwa kwenye hifadhi ya barabara ya Mwendokasi.

Amesema hayo leo August 19,2025 baada ya kuchukua fomu ya kugombea Ubunge katika Jimbo hilo kutoka kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi Temeke Bi.Fortunata Shija huku akibainisha kuwa mradi huo umejengwa bila kufuata taratibu,na Serikali imeshindwa kumchukulia hatua mwekezaji huyo.

Aidha amesema kuwa nyumba hizo zimejengwa kwenye eneo la barabara ya Chamazi-Kongowe ambapo umepita mfereji wa Maji taka,Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na kituo cha Mabasi ya Mwendo kasi.

“Mimi ni Mwananchi wa kawaida kabisa,shida zote za Mbagala nazifahamu,lakini nimeona wakati wa uchaguzi nisibaki tu kua vilevile basi niwe Mgombea kwasababu hakuna mtu mwingine anayeweza kusawazisha zile shida,

nawambia Wananchi wenzangu wa Mbagala mti dawa(Mbunge)unakuja tuchaguane sisi wenyewe Wananchi tuachane na habari za viongozi,viongozi hawajatufikisha pale sisi tunapotaka.” amesema Ndonga

“Mbagala kwasasa tunahitaji kuwa na Mwendokasi,fununu zinaonekana mradi wa Mwendokasi utakapoanza nauli itakua bei juu,kuliko daladala hatuwezi kuwa na Serikali ya namna hiyo,tunahitaji Mwendokasi uwe rahisi kuliko daladala kwasababu ni taasisi ya Umma.”

Amesema kuwa kwenye mradi huo Benki ya Dunia(WB)imewekeza katika zile barabara,huku Wananchi ndo wanaolipa kodi,hivyo nauli inatakiwa kuwa rafiki kwa Wananchi ili waendelee kufanya shughuli zao za kila siku za kuwaingizia kipato.

“Haiwezekani leo gari la Ndonge nauli shilingi mia sita hadi Kariakoo halafu unatuletea Mwendokasi una tuambia tulipe elfu moja(1,000) au elfu moja na mia tano(1500),wakati kipato chetu ni kilekile na Maisha yetu ni yaleyale.”amesema.

Ameendelea kusema kuwa Mbagala kuna kero nyingi ikiwemo Miundombinu ya Barabara,nakwamba Wananchi wa Mbagala wanao fanya Biashara zao barabarani wanafukuzwa,lakini kuna Mwekezaji kajenga fremu za biashara katika kituo cha Mwendokasi kinyume na taratibu bila kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.

“Kuna mtu kajenga barabarani na anapangisha kwahiyo tutatafuta jibu kwamba ukiwa na fedha ukijenga flemu barabarani unakua halali,lakini kama hauna fedha ukaweka Biashara barabarani sio halali,hii haiwezekani na hatutakubali watu wa Mbagala.”amesema

Nakusisitiza kuwa”Lazima tuhakikishe kwamba kama sisi wafanyabiashara tunatoka barabarani basi tunaenda kuweka pale mbele ya fremu na tusione mgambo au mtu yeyote kwasababu anaekaa kwenye fremu anafanya makosa na aliyetandaza biashara zake pale barabarani anafanya makosa,wana Mbagala tushikamane matatizo yetu hakuna mtu mwingine ambaye atakuja kututatulia,tuachane na habari za viongozi.