Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewapa tuzo washindi watatu wa mazingira challenge shindano lililoandaliwa maalum na baraza kwaajili ya kuhamasisha uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Washindi hao walikadhiwa tuzo zao jana na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Cyprian Luhemeja. kwenye Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza kabla ya kutoa tuzo hizo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi alisema Baraza lilianzisha shindano hilo kama sehemu ya kampeni zake kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira nchini.
Alisema NEMC iliwaomba wananchi wapige wapiga eneo ambalo mazingira yake yamehifadhiwa na kutunzwa vizuri ambayo itawahamasisha wengine kutunza mazingira.
Dk Semesi alimtaja mshindi wa kwanza kwenye shindano hilo kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Theofil Kisanji cha jijini Mbeya ambaye ni Mwenyekiti na Mwanzilishi wa klabu ya Mazingira chuoni hapo.

Alimtaja mshindi wa pili kwenye shindano hilo kuwa ni Magdalena Chuma, ambaye amepanda miti mingi nyumbani kwake Mbagala Chamazi ambayo imestawi vyema na kusaidia kutoa hewa safi na kivuli kwa familia na jamii nzima inayomzunguka.
Alisema Magdalena amekuwa balozi wa mazingira katika eneo lake kwa kuhamasisha watu wanaomzunguka kutunza mazingira ambayo watu wengi wamehamasika na kupanda miti.
Alimtaja mshindi wa tatu kwenye shindano hilo kuwa ni Stanley Urassa ambaye ni kiongozi wa vijana 17 wanaojihusisha moja kwa moja na shughuli za kutunza na kuhifadhi mazingira .
Alisema shughuli zinazofanywa na kundi la vijana hao ni pamoja na urejelezaji wa taka, kampeni za usafi wa mazingira, upandaji wa miti na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu masuala yanayohusu mazingira.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mhandisi Luhemeja alisema utunzaji wa mazingira ni muhimu kwaajili ya kupunguza ongezeko la gesi joto duniani hivyo aliwataka wananchi wabadilike na wayape kipaumbele mazingira.
Alisema serikali kwa upande wake imejitahidi kupiga marufuku uingizaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki nchini kama sehemu ya kuhifadhi na kutunza mazingira nchini.
Alisema serikali imeupa kipaumbele mkakati wa matumizi ya nishati safi ili kuondokana na matumizi ya kuni mkaa ambayo yanaweza kuifanya nchi kuwa jangwa na kusababisha kukosekana kwa mvua na kuleta jangwa.
“Niwapongeze Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tantrade, mwaka jana kulikuwa na uchafu maeneo mengi ndani ya maonyesho haya lakini leo nimezunguka ni kusafi sana na nawapa changamoto mpande miti zaidi ili kuwe na msitu ndani ya viwanja hivi,” alisema
