Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Dar es salaam

Ikiwa imesalia siku kadhaa ya kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika Machi 8 kila mwaka Ngome ya Wanawake ya Chama cha ACT-Wazalendo imesema siku hiyo wataifanya kwa kipekee kwa kuweka tabasamu kwa makundi ya Yatima wajane,Wazee na kutoa Damu,na kufanya ibada ya kukumbuka watu waliopoteza maisha wakati wa ghasia zilizotokea Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 26, 2026, katika Makao Makuu ya chama Magomeni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ngome hiyo, Janeth Rite, amesema hawana sababu ya kusherehekea siku hiyo kwa sherehe wakati bado kuna majonzi miongoni mwa Watanzania waliopoteza wapendwa wao, huku wengine wakibaki na ulemavu wa kudumu.

Amesema Machi mwaka huu utakuwa mwezi wa maombolezo kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho.

Kwa mujibu wa Janeth, Machi 8, 2026 watatumia siku hiyo kufanya maombi na hitma, pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutembelea wazee na watoto yatima, kufanya usafi katika vituo vya afya, kutoa misaada, kuchangia damu, kuzuru makaburi na kufanya mikutano mikubwa ya hadhara nchi nzima wakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Machozi ya Mama ni Deni la Taifa.”

Rite amesisitiza kuwa Ngome ya Wanawake ACT-Wazalendo itaendelea kuwa sauti ya wasiojiweza na kwamba hawatanyamaza hadi haki itakapotendeka.