*Awataka wananchi kujiunga ili kuwa na uhakika wa matibabu

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tabora

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Bw. Rogath John Mboya ameahidi kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), katika kuhamasisha kujiunga na huduma zake ili wajihakikishie huduma za matibabu wakati wote bila kikwazo cha fedha.

Amesema kuwa ameshuhudia NHIF ikiokoa maisha ya mtoto wake wakati alipopatwa na maradhi yaliyohitaji uchunguzi wa kitaalam na wenye gharama kubwa.

Haya ameyasema leo wakati akizungumza na Bodi ua Wakurugenzi na Menejimenti ya NHIF katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambapo Bodi hiyo ilifika ofisini hapo kwa lengo la kuweka mikakati ya mashirikiano ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote na kuimarisha mahusiano.

“Suala la kuwa na Bima ya Afya ni suala muhimu kwa wananchi wote na kama hujapatwa na changamoto kubwa za maradhi huwezi kuelewa umuhimu wake, binafsi nimeona NHIF ikiokoa uhai wa mwanangu hivyo tuko tayari kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kujiunga,” alisema Bw. Mboya.

Alisema kuwa mchango wa NHIF katika sekta ya afya ni mkubwa hivyo akaupongeza uongozi wa Mfuko kupitia Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka kwa jitihada kubwa za maboresho yaliyofanyika katika huduma zake ambapo kwa sasa mwanachama anapata huduma kwa urahisi na kwa ubora mkubwa.

Kwa upande wa Bodi ya Wakurugenzi iliyoongozwa na Kaimu Mwenyekiti Bi. Zubeda Chande aliushukuru uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Tabora kwa kukubali kushirikiana na NHIF katika kuhakikisha suala la Bima ya Afya kwa Wote linatekelezeka na ndoto ya Serikali ya kila mwananchi kuwa na bima ya afya inakuwa halisi.

“Kipaumbele chetu kama Bodi ni kuona maelekezo ya Serikali yanatekelezwa ili kila mwananchi aweze kunufaika na uwekezaji uliofanyika katika sekta ya afya kwa kupata huduma za matibabu kupitia mfumo wa bima ya afya hivyo tunashukuru sana kwa kuwa tayari kushirikiana na sisi katika hili,” alisema Bi. Chande.

Naye Mkurugenzi Mkuu Dkt. Isaka alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma bora za matibabu na akaahidi kuendelea kufanya maboresho ya kihuduma ili wananchi waweze kuzifikia huduma za Mfuko ikiwemo usajili na matibabu kwa urahisi zaidi.

Wajumbe wa Bodi walioshiriki ziara hiyo ni Bw. Shabaan Kabunga na Bw. Amour Amour ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango Wizara ya Afya.