Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Lugubu, Kata ya Lugubu Wilayani Igunga Mkoani Tabora amepoteza maisha na watoto wake wanne baada ya kunywa sumu aina ya ruruka 80WDG itumikayo kuulia viwaji jeshi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo juzi majira ya saa 10 jioni katika Kitongoji cha Lugubu, Kijiji cha Lugubu katika kata hiyo.

Alisema kuwa mama huyo alinunua pakiti moja ya dawa hiyo ambayo ni sumu ya kuulia wadudu na kuikoroga kwenye kikombe cha chai kisha akawanywesha wanawe wote na yeye mwenyewe akanywa, wote wakapoteza maisha.

Kamanda alifafanua kuwa mwanamke huyo alichukua hatua hiyo baada ya mume wake kwenda shambani huku yeye akibaki na watoto nyumbani, na kubainisha chanzo cha tukio hilo kuwa ni wivu wa mapenzi baina ya wanandoa hao.

Alitaja jina la mama aliyeua wanawe na kujiua mwenyewe kuwa ni Kang’wa Tungu Mahigi (25) mkulima mkazi wa Kitongoji cha Lugubu na wanawe ni Sengi James (8), Simon James (6), Elisha James (3) na Kashinje James (miezi 7).

Alidokeza kuwa wakati wa uchunguzi wa tukio hilo walikuta pakiti ya sumu hiyo nyumbani kwa marehemu ambayo ilikuwa imetumika pamoja na kikombe cha chai chenye sumu yenyewe, baada ya uchunguzi miili ilikabidhiwa kwa wanandugu.

‘Hili ni tendo la kikatili, kihalifu na lisilo na utu, watoto wasio na hatia wameangamizwa pasipo sababu yoyote, hasira, wivu na ukatili wa namna hii haukubaliki katika jamii’, alisema.   

Kamanda alilaani matukio ya namna hiyo na kutoa wito kwa jamii kutumia viongozi wa dini, serikali, dawati la jinsia na watoto katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao.