Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amesema ni jambo la faraja kuona Benki ya NMB inaendelea na utaratibu wake wa kuwakutanisha pamoja wateja wake, wadau na watoto yatima kwa lengo la kupata Iftari ya pamoja jambo linaloleta furaha miongoni mwao.
Ameyasema hayo mara baada ya Iftari iliyoandaliwa na Benki ya NMB katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Amesema hatua ya Benki ya NMB kuftari pamoja na Wateja wake na watoto yatima inadhihirisha kuwa benki hio si tu Taasisi ya kifedha bali ni mdau muhimu katika ustawi wa jamii na maendeleo kwa ujumla.
Alhajj Hemed amefahamisha kuwa Benki ya NMB imekuwa mdau wa maendeleo nchini kwa kuchangia katika ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo lakini pia kushirikiana na wananchi katika shughuli za kijamii hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila aina ya mashirikiano ili Benki hio na nyenginezo ziweze kufanya kazi zao bila ya usumbufu wa aina yoyote.
Hata hivyo, Alhajj Hemed amewaasa waumini wa dini ya kiislam na wananchi kwa ujumla kuendeleaza upendo, ukarimu, kusaidiana na kuyafanyia kazi mafundisho yanayopatikana katika mwezi wa ramadhani na kuyaendeleza hata baada ya kumalizika kwa Ramadhani ili kuweza kupata mafanikio mema hapa duniani na kesho akhera.
Sambamba na hayo, Alhajj Hemed amesema mwezi wa ramadhani ni chuo chenye kuzitakasa nyoyo kiimani na kinachofunza nidhamu, matendo ya kheri, kuepuka maovu, kukithirisha ibada na kuomba msamaha kwa Allah ili kuweza kupata radhi zake kama lilivyo lengo la kufunga.
Aidha, amesisiatiza suala zima la kudumisha Amani, umoja na mshikamano pamoja na kuwaombea dua viongozi ili waweze kutimiza azma yao ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bibi RUTH ZAIPUNA amesema Benki ya NMB imekuwa ikiandaa Iftari inayojumuisha watendaji wake na wadau mbali mbali kwa lengo la kuendeleza mahusiano mema baina yao lakini pia kurejesha shukurani kwa wadau ambao wanaendelea kufanya kazi na Benki hio.
Bibi ZAIPUMA amefahamisha kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaonesha uhalisia na thamani ya kuishi katika misingi ya upendo, kusaidiana, kuhurumiana, uvumilivu na kuheshimiana jambo linalosaidia kulinda maadili katika jamii kutokana na watu kuwa karibu na Mwenyezi Mungu.
Aidha, amesema Benki ya NMB itahakikisha inaifikia jamii katika nyanja mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo kutoa misaada hasa katika kipindi hiki cha Ramadhani ili kutoa unafuu katika kuitekeleza vyema ibada hio ya funga.
Benki ya NMB imedhamiria kuyafikia makundi mbali mbali yenye mahitaji maalum Tanzania ambapo kwa kipindi hiki cha Ramadhani wanatarajia kuwafikia watoto yatima zaidi ya 50 kutoka katika vituo mbali mbali vya kulelea watoto yatima.
Katika Iftari hio Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakabidhi zawadi zilizoandaliwa na Bank ya NMB kwa watoto yatima kutoka katika vituo vya kulelea watoto cha ASSALAAM NA KIDUNDO ORPHANAGE CENTER kwa lengo la kuonesha upendo na kuwajengea furaha watoto hao.







