Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid J. Maulid, ameeleza nidhamu na uwajibikaji ni chachu ya mafanikio katika sekta ya elimu
Kauli hiyo aliitolewa 25 Juni, 2025 wakati akifungua mafunzo ya Utawala Bora katika Elimu kwa Maafisa Elimu Kata 352 kutoka mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro mafunzo ambayo yamefanyika ADEM Bagamoyo kuanzia tarehe 25 hadi 27 Juni, 2025, na kufadhiliwa na Mradi wa BOOST chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha Maafisa Elimu Kata kusimamia kwa ufanisi shughuli za elimu katika ngazi ya kata, ili kuhakikisha ubora wa elimu unaimarika kuanzia ngazi ya jamii.
Dkt. Maulid alieleza kuwa Maafisa Elimu Kata wana jukumu kubwa la kutafsiri na kutekeleza kwa vitendo maono ya Serikali kuhusu mageuzi katika sekta ya elimu, hususan kupitia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2013 (Toleo la 2024) na mtaala ulioboreshwa.
“Mabadiliko na mageuzi yanayotarajiwa kupitia utekelezaji wa sera na mtaala mpya yako mikononi mwenu kama wasimamizi wa kwanza wa elimu katika ngazi ya kata.

“Tunatarajia kuona matokeo chanya kuanzia ngazi ya shule hadi kata, kwa kusimamia ipasavyo yale mtakayojifunza katika mafunzo, ambapo ndiyo yatakuwa dira ya ufanisi katika usimamizi wa elimu,” alisema Dkt. Maulid.
Dkt. Maulid aliwataka Maafisa Elimu Kata kusoma, kuelewa, na kutekeleza ipasavyo miongozo yote inayotolewa na mamlaka zinazohusika na elimu nchini, ikiwemo Ofisi ya Kamishna wa Elimu, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi .
Alisisitiza umuhimu wa kusimamia nidhamu, uwajibikaji, ufundishaji na ujifunzaji bora mashuleni, ili kuinua ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wa Kitanzania.
Nae Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Dkt. Alphonce Amuli, alieleza kuwa washiriki wa mafunzo hayo watajengewa uwezo katika maeneo mbalimbali.

Alieleza maeneo hayo ni pamoja na uongozi, usimamizi na utawala katika elimu; utawala bora katika elimu; uandaaji wa mpango wa jumla wa maendeleo ya elimu katika ngazi ya serikali za mitaa; ufuatiliaji na usimamizi wa shule; usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya shule; ukaguzi wa ndani na ushirikishwaji wa jamii na utatuzi wa malalamiko katika sekta ya elimu.
